KOCHA Mkuu wa Simba, Joseph Omog, amemwangalia beki wake Mganda, Juuko Murshid na kuamua kumpa programu maalumu ili arudi kwenye kiwango chake.
Juuko ambaye amerejea kutoka Uganda alipokuwa kwenye timu yake ya Taifa ya ‘Uganda Cranes’ ambayo imefunzu kucheza ‘Afcon’, ameanza mazoezi mepesi kwa ajili ya mchezo wao wa kesho dhidi ya Azam.
Kwenye mazoezi ya juzi yaliyofanyika kwenye Uwanja wa Boko Veterani, Juuko alipewa mazoezi ya kuzunguka uwanja na baadaye kupumzishwa kwa ajili ya kuanza programu nyingine.
Meneja wa Simba, Mussa Hassan ‘Mgosi’, alisema zoezi la kukimbia alilofanya Juuko ni programu maalumu aliyopewa na mwalimu.
Alisema Omog ametoa programu hiyo kwa kuwa Juuko hakuwa na wenzake kwenye kikosi hicho kwa muda mrefu hivyo lazima ajifue kivyake.
“Yale ni mazoezi ambayo Omog alitoa kwa Juuko kama programu maalumu na leo yamemalizika na huenda akajumuika na wenzake kwenye mazoezi ya uwanjani,” alisema.
Akizungumzia maandalizi yao kwenye mchezo wa Jumamosi, Mgosi alisema sehemu kubwa inayofanyiwa kazi ni safu ya ushambuliaji ambayo imekuwa na tatizo la kukosa mabao mengi.
“Mwalimu amekuwa kwenye programu maalumu ya mazoezi ambayo amekuwa akiifanyia kazi ila kikubwa ni pointi tatu tu kwenye mchezo huo,” alisema.
Post a Comment