KUFUATIA kufunga bao pekee katika mchezo wa juzi
Jumamosi dhidi ya Azam FC, kiungo mshambuliaji wa Simba, Shiza Kichuya ametuma
salamu akisema anaisubiri Yanga.
Kichuya ambaye sasa ni mmoja wa wachezaji
wanaopendwa na mashabiki wa Simba, ametamba kuwa wapo tayari kucheza na Yanga wakati wowote kuanzia sasa kutokana na
ubora wa kikosi chao na kamwe hawawezi kuwahofia.
Simba na Yanga zinatarajiwa kukutana Oktoba Mosi
katika mchezo ambao umeshavuta hisia za wengi. Timu zote zipo kwenye ubora wa
aina yake, Yanga waliwafunga Mwadui mabao 2-0 wakiwa ugenini kwenye Uwanja wa
Kambarage, Shinyanga, juzi.
Simba iliifunga timu ngumu zaidi ya Azam FC bao
1-0 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar, huku Kichuya akifunga bao hilo pekee kwa
ustadi mkubwa.
Kichuya aliyejiunga na Simba akitokea Mtibwa
Sugar kwa mkataba wa miaka miwili, amefanikiwa kucheza michezo yote mitano akiwa
na kikosi cha Simba na kufanikiwa kufunga mabao mawili mpaka sasa.
Kichuya alisema kuwa hawawezi kuwahofia Yanga
hata kidogo na wapo tayari kucheza nao wakati wowote kwani amekuwa akimuomba
Mungu amuongoze kufunga mabao katika kila mchezo anaocheza.
“Unajua nimekuwa nikijituma kila siku ili niweze
kufunga mabao, sasa nashukuru nimeweza kufunga kwa sababu nimekuwa nikimuomba
kila siku niwe nafunga kitu ambacho kimetokea leo (juzi) maana ukiangalia Azam
ndiyo walikuwa wapinzani wetu lakini kwa kuwa tumewafunga sisi ndiyo tunaongoza
ligi.
“Kilichobaki kwetu ni kuendelea kupambana kwa
sababu suala la kupata ubingwa lipo wazi kabisa kutokana na kikosi ambacho
tunacho, mechi bado nyingi sana, tunajua baada ya kucheza na Majimaji tutacheza
na Yanga lakini hatuwezi kuwahofia, waje tu, maana tupo tayari kwa lolote,”
alisema Kichuya.
Kichuya aliongeza kuwa tangu walipoanza kuutumia
Uwanja wa Uhuru kwa mechi za Ligi Kuu Bara, kuna ahadi aliiweka moyoni ambayo
juzi Jumamosi aliitimiza.
Kichuya alipofunga bao alikwenda moja kwa moja
kwenye bango lililokuwa kusini mwa uwanja huo likiwa na picha ya kiungo wa
zamani wa Simba, Patrick Mafisango na kupiga saluti.
Ameliambia gazeti hili kuwa, Mafisango alipokuwa
akiichezea Simba, alikuwa ni mchezaji anayempenda zaidi na ndiyo maana juzi
akamuenzi kwa staili hiyo.
“Kila siku nilikuwa naliona lile bango likiwa na
picha ya Mafisango, nikasema endapo siku nikifunga bao basi lazima niende
kushangilia pale.
“Kama uliniona nilipofunga nilitaka kwenda
kushangilia walipokuwa mashabiki, lakini nilipokumbuka ile ahadi yangu, moja
kwa moja nikaenda lilipo lile bango ambalo nilikuwa naliona kila siku, nikapiga
saluti, watu wengi wanadhani nimewapigia saluti mashabiki, kumbe nilimpigia
Mafisango ambaye kiukweli nilikuwa nampenda sana,” alisema Kichuya.
Ikumbukwe kuwa, Mafisango ambaye alikuwa raia wa
Rwanda mwenye asili ya DR Congo, alifariki dunia Mei 17, 2012 kwa ajali ya gari
akiwa jijini Dar. Kiungo huyo alijiunga na Simba mwaka 2011 akitokea Azam FC.
Post a Comment