USHINDI wa
mabao 4-0 walioupata Simba kwenye mchezo wao juzi dhidi ya Majimaji, umewapa
kiburi timu hiyo na kuamua kuwaita mashabiki wa Yanga kwenda kwa wingi Uwanja
wa Taifa Oktoba mosi, timu hizo zitakapokutana.
Wito huo
umetolewa na Kocha Msaidizi wa Simba, Jackson Manyanja, ambaye aliwataka
mashabiki hao wa Yanga kuhudhuria kwa wingi mpambano huo kwani wanaamini
wataibuka na ushindi.
Akizungumzia
maandalizi yake kuelekea mchezo huo, Mayanja alisema kikosi chake kipo sawa,
huku lengo likiwa moja tu ambalo ni ushindi.
“Tunapaswa
tukubali hii ni mechi kubwa, hivyo kama tungepoteza mchezo wetu na Majimaji,
morali ingeshuka kwa wachezaji na hata mashabiki, hivyo ushindi huu umetupa
morali kubwa zaidi ya pambano letu na Yanga,” alisema.
Mayanja
alisema Simba sasa iko tayari kuwakabili
Yanga kwa kuwa kikosi kimeiva na wana uhakika wa kushinda mechi hiyo, na kwa
wapenzi wa Yanga waliozoea kuionea Simba, wafike Taifa kushuhudia
kitakachowakuta.
“Msimu
uliopita, nilipewa jukumu la kuinoa timu na sikuwa na muda mzuri kama huu wa
sasa, kwa sasa tuko vichwa viwili na Joseph Omog, nadhani mnaona
kinachoendelea,” alisema Mayanja.
Alisema
kamati ya usajili chini ya mwenyekiti wake, Zacharia Hanspope, imefanya kazi
kubwa ambapo Simba msimu huu kamwe haitegemei mchezaji mmoja.
“Kwenye
mpira lolote linaweza kutokea, lakini sisi tunachojivunia zaidi ni kuwa na
wachezaji wengi zaidi ambao wote wana uwezo wa kubadili matokeo na hatutegemei
mchezaji mmoja, mfano alipoingia Mohammed Ibrahim wote mliona ni jinsi gani alibadilisha
mchezo,” alisema.
“Mtakumbuka
mwaka jana tulikuwa na tatizo la wachezaji, hata mechi yetu ya mwisho
tuliocheza na Yanga tulimpanga Abdi Banda kama beki wa kati, lakini sasa tuna
wachezaji kila sehemu,” alisema.
Alipoulizwa
ni mchezaji gani ndani ya kikosi cha Yanga anayemhofia, Mayanja alisema
wachezaji pekee anaowahofia ni nyota wake wa Simba ambao ndio watakaoleta
matokeo kwenye mchezo huo.
“Mechi hiyo
ni kama fainali, hakuna tunayemhofia Yanga, nawaogopa nyota wangu wa Simba
ambao ndio watakaoleta matokeo siku hiyo,” alisema.
Alisema
atalifanyia kazi tatizo la uchoyo la wachezaji wake linalojitokeza kwenye
michezo mbalimbali mpaka sasa.
“Hili suala
lazima tulifanyie kazi mapema kabla halijakuwa, mtu akifunga bao si lake ni la
timu nzima, hivyo ni jambo ambalo wanapaswa kulijua na tunalifanyia kazi,”
alisema.
Post a Comment