PAMBANO la watani wa jadi, Simba na Yanga huwa lina raha yake. Kabla ya pambano hili huwa kuna mambo mengi yanafanyika ikiwemo vikao vya siri  ilimradi tu timu ipate ushindi.
Kuelekea katika pambano hilo la Oktoba mosi, Simba wameanza mchakato mapema hasa kwa lengo la kuhakikisha msimu huu wanafuta uteja wao kwa Yanga baada ya msimu uliopita kugawa pointi zote sita kwa kuruhusu kuchapwa mabao manne yaani mawili kwa kila mechi.
Taarifa za ndani ya klabu hiyo zinasema kuwa kambi ya mwaka huu itakuwa tofauti na msimu uliopita ambapo wamedhamiria kufanya mambo yao kimya kimya ili kuogopa siri zao kuvuja.
Chanzo hicho kiliendelea kusema kuwa kumekuwa na vikao vya siri ambavyo vinaendelea vikiwa na lengo la kupanga mikakati ya kuwamaliza wapinzani wao siku hiyo.
Wekundu hao wa Msimbazi ambao walikuwa na desturi ya kwenda Unguja kujiandaa na watani wao Yanga, imeelezwa safari hii hawatakwenda Unguja na badala yake watakwenda kujificha katika kambi ya siri wakifanya mazoezi bila kuonwa na mashabiki.
Kutokana na umuhimu wa mchezo huo, imeelezwa kwamba hawatakwenda visiwani humo, baada ya kusikia Yanga wanakwenda kuweka kambi yao kisiwani Pemba kujiandaa na mchezo huo.
Mchezo huo utakuwa wa kwanza kwa kocha Joseph Omog tangu arejee nchini kuifundisha Simba ambayo inaongoza ligi ikiwa imejikusanyia pointi 13.
Omog aliondoka hapa nchini mara baada ya kutupiwa virago na Azam FC aliowapa kombe la Ligi Kuu Tanzania Bara kwa mara ya kwanza na kuweka historia katika kikosi hicho tangu kilipoanzishwa.
 Chanzo chetu kimesema kuwa vigogo wakiwemo Friends of Simba, wanatarajiwa kukutana leo kwa ajili ya kupanga mikakati kadhaa kuelekea katika pambano hilo.
“Kesho (leo) mabosi wanakutana, nia na madhumuni ni kujadili juu ya mchezo na Yanga lakini pia wamempa jukumu kocha kuchagua sehemu ambayo anaona inafaa kwa ajili ya kuweka kambi yenye utulivu,” kilisema chanzo hicho.
Chanzo hicho kiliendelea kueleza kuwa hapo awali kocha Omog aliwaambia viongozi hao anataka kambi ya timu hiyo ikawekwe Morogoro katika Chuo cha Biblia.
“Awali kocha alipendekeza timu irudi Morogoro, lakini viongozi naona ndio wanafanyia kazi mapendekezo hayo ya kocha kama wataenda huko au vipi,” kiliendelea kusema chanzo hicho.
Chanzo hicho kilisema kuwa sababu ya Omog kutaka kwenda kuweka kambi Morogoro ni pamoja na mazingira ya sehemu hiyo kuwa ni mazuri lakini pia haitakuwa rahisi kwa shabiki au mtu yeyote kuingia ndani kushuhudia mbinu za kocha huyo.
 CHANZO: BINGWA

Post a Comment

 
Top