YANGA wanaweza kuishangaza Simba kwa mara nyingine, baada ya kuwa katika mipango kabambe ya kumsajili kiungo wa zamani wa Wekundu hao wa Msimbazi, Mzimbwbwe Justice Majabvi.
Hatua hiyo ya Yanga kuwa katika mipango hiyo inatokana na tatizo lililopo katika eneo la kiungo mkabaji linalowasumbua ambapo wameona Majabvi anaweza akafiti.
Simba waliachana na kiungo huyo baada ya kudai mwenyewe kuwa anakwenda nchini Australia kuishi na mkewe ambaye anafanyia kazi huko na taarifa hizi za Yanga kumnyemelea zinaweza kuwa mbaya kwa Wanamsimbazi hao.

Anayetajwa kama atampisha Majabvi ni Mbuyu Twitte au Obrey Chirwa, ambaye ameshindwa kuwashawishi mashabiki na kama ataendelea kusuasua panga hilo linaweza kumpitia.
Kigogo mmoja wa Yanga amesema kuwa wapo kwenye mchakato wa kumfuatilia Majabvi, ambaye pia anamudu kucheza namba zaidi ya moja na kama mambo yatakwenda vizuri, anaweza akawa ingizo jipya dirisha dogo la usajili.
“Hizo taarifa ni kweli zipo, lakini bado hatujaanza mazungumzo rasmi, unajua tuna tatizo nafasi ya kiungo mkabaji, ndiyo maana tunahangaika kupaimarisha, kama mambo yatakaa vizuri huenda tukamfuata huko aliko na kumsajili dirisha dogo,” alisema.
Mbali na Majabvi, pia Wanajangwani hao bado hawajakata tamaa ya kumsajili aliyekuwa pacha wa Donald Ngoma walipokuwa FC Platinum, Walter Musona, ambaye taarifa zinadai kuwa yupo mbioni kumaliza mkataba wake ambapo itakuwa rahisi kwa Yanga kumnasa.

Post a Comment

 
Top