KUREJEA kikosini kwa beki, Vincent Bossou na kiungo Haruna Niyonzima ambao walikosa mchezo wa juzi wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL), dhidi ya Ndanda FC uliomalizika kwa suluhu, kumeanza kuipa kiburi Yanga kuelekea kwenye pambano lao dhidi ya Majimaji ya Songea.
Bossou na Niyonzima walichelewa kurudi kuungana na wenzao kwa ajili ya pambano dhidi ya Ndanda lililopigwa kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona kutokana na kuwa na majukumu katika timu zao za Taifa.


Akizungumzia mchezo ujao dhidi ya Majimaji, Kocha Msaidizi wa Yanga, Juma Mwambusi, alisema anaamini kuwa Bossou na Niyonzima wataongeza nguvu kwenye kikosi chao kwenye mchezo wa Jumamosi dhidi ya Majimaji, katika Uwanja wa Uhuru.
“Tumepata sare na wote mmeona imetokana na uwanja mbaya hivyo sasa tunahamisha silaha zetu kwenye mchezo unaofuata dhidi ya Majimaji,” alisema Mwambusi: “Tunashukuru Bossou na Niyonzima wamerudi tuna imani tutakuwa nao pale kwenye Uwanja wa Uhuru.”
Kuhusu majeruhi, Geofrey Mwashiuya, Pato Ngonyani, Malimi Busungu, Mwambusi alisema wanaendelea vizuri na kwa upande wa kipa wao Deogratius Munishi ‘Dida’ aliyekuwa kwenye msiba wa baba yake mzee Munishi naye anatarajia kurejea kikosini.

Post a Comment

 
Top