KOCHA Mkuu wa Mwadui FC, Jamhuri Kihwelo ‘Julio’,
amesifu kiwango kilichoonyeshwa na Yanga katika mchezo wa ligi kuu dhidi ya
timu yake ambapo walilala kwa mabao 2-0.
Yanga, juzi iliifunga Mwadui katika mchezo mkali
uliopigwa Kambarage. Mabao ya Yanga yalifungwa na Amissi Tambwe na Donald
Ngoma, ushindi huo umeifanya Yanga kutinga nafasi ya pili ikiwa na alama 10,
anayeongoza kwenye msimamo ni Simba ambayo ina alama 13.
Julio alisema Yanga ilionyesha soka safi na hiyo
ilitokana na kutoka kushiriki kwenye michuano ya kimataifa (Kombe la
Shirikisho) ambapo bado wachezaji wake walionekana kuwa na ari kubwa na kucheza
kwa kuonana muda wote uwanjani huku akishindwa kujizuia na kulisifia bao la
pili lililofungwa na Donald Ngoma aliyepokea pasi kutoka kwa Simon Msuva.
Julio ambaye wakati wa mapumziko alitenganishwa
na Kocha wa Yanga, Hans Pluijm baada ya kutaka kuzichapa, juzi alishindwa
kujizuia na kujikuta akitoa lawama za wazi kwa mabeki wake kuwa walicheza
kizembe na kusababisha kupoteza mchezo huo.
“Niwapongeze Yanga, wana kikosi kizuri sana,
wanacheza kwa kuonana, nafikiri kwa kuwa wametoka kushiriki michuano ya
kimataifa, wana timu nzuri lakini kikubwa ambacho kimeniangusha ni uzembe wa
mabeki wangu, walikosa umakini. Nitafanyia kazi upungufu huo ili tuweze kufanya
vizuri katika mchezo unaofuata,” alisema Julio.
Post a Comment