ZIKIWA bado siku chache miamba ya
soka hapa nchini, timu za Simba na Yanga zikutane uwanjani katika Ligi Kuu
Bara, Katibu Mkuu wa Baraza la Wazee wa Yanga, Ibrahim Akilimali amewasifia
wapinzani wake hao kuwa wapo vizuri.
Akizungumza na Championi Ijumaa juu
ya mchezo huo wa Oktoba Mosi, mwaka huu, Akilimali alisema msimu huu Simba ina
kikosi kizuri, imejitahidi kusajili wachezaji wazuri tofauti na msimu uliopita
na kudai wakiwa makini wanaweza kutoa ushindani kwa Yanga lakini bado anaamini
Yanga itaibuka na ushindi katika mchezo huo wa wiki ijayo.
“Kuna mambo ambayo nimezushiwa hivi
karibuni kuwa eti nilikutana na viongozi wa Simba kujadili mchezo wa Oktoba Mosi,
hao waliosema hivyo wana lao jambo.
“Ukweli ni kwamba, sijafanya kikao na
kiongozi yeyote wa Simba na siku hiyo inayosemwa mimi nilikuwa Bagamoyo
nikiuguza maumivu ya jino ambalo lilikuwa likisumbua lakini tayari nimeshaling’oa
na sasa nipo kwangu hapa Dar, waniache, wasitake kunipaka matope kwa sababu tu
ya msimamo nilionao juu ya Yanga kukodishwa.
“Kuhusiana na mechi yetu na Simba
itakuwa na ushindani mkubwa msimu huu kutokana na usajili mzuri ambao Simba
wamejitahidi kufanya, nawatabiria kuwa safari hii watapiga hatua kidogo kutoka
nafasi ambayo msimu uliopita waliishika lakini pia watatoa upinzani kidogo
katika mchezo wetu kama viongozi wao watajipanga.
“Lakini suala la kupata ushindi
katika mchezo huo hilo wasahau kabisa kwani tutawafunga, hapo awali baada ya
Simba kutufunga mabao 5-0 niliwahi kusema kuwa tutalipa kisasi kwa kuwafunga
mabao mawili kila tutakapokutana nao ambapo mpaka sasa tumeshawafunga manne,
hivyo siku hiyo pia tutawafunga mawili na kuwaacha na deni la bao moja,”
alisema Akilimali.
Post a Comment