SIMBA imeonekana kudhamiria kulipa kisasi katika mechi ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Yanga itakayochezwa Oktoba Mosi, mwaka huukwa kuandaa wachezaji wawili maalumu kwa mchezo huo.
Mchezo huo, wenye upinzani mkubwa, utachezwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam. Simba haikuwahi kuwatumia straika Ame Ali na kiungo Mussa Ndusha, sasa inataka kuwapa kazi maalumu kwa Yanga.
Kocha wa Simba, Joseph Omog ambaye timu yake itaweka kambi Morogoro kujiandaa na mechi hiyo, amepiga hesabu na kuona Ame anamudu kucheza soka la kibabe kwa mabeki wanaocheza kindava kama wale wa Yanga ambao ni Kelvin Yondani, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, hata Vincent Bossou.
Omog alisema: “Ame Ali ana mwili mkubwa wa kuweza kupambana na mabeki wa Yanga,nadhani atakuwa msaada kwetu siku ya mechi yetu.
“Hii haimaanishi waliopo ni wabovu, hapana ila Ame ni mpambanaji na ataweza kukabiliana na mabeki wa Yanga kutokana na mechi yenyewe ilivyo.”

Japokuwa Omog, raia wa Cameroon, hakuweka wazi, gazeti hili linafahamu kuwa, ameamua kumtumia Ame baada ya kuona Laudit Mavugo na Ibrahim Ajib kutokuwa wapambanaji kwa mabeki wakorofi.
Pia Omog amepanga kumtumia kiungo mkabaji raia wa DR Congo, Ndusha ambaye hadi kufikia wiki ijayo hati yake ya uhamisho wa kimataifa (ITC) itakuwa imeshafika.
"Upo uwezekano mkubwa wa kumtumia Ndusha kwenye mechi na Yanga, kwani tunatarajia kupata ITC yake mapema wiki ijayo, huyu naye atakuwa mtu maalumu kwetu,” alisema Omog.
Naye Menejawa Simba, Mussa Mgosi alisema amemuweka kitimoto Mavugo akimtaka abadilike haraka kutokana na aina yake ya uchezaji.
"Mavugo jana (juzi) nilifanya naye kikao na kumtaka abadilike kwa haraka kutokana na aina yake ya uchezaji ya upole mara watakapokutana na Yanga kwani wapinzani wetu wana mabeki wanaocheza kibabe.
"Nimemwambia kuna Yondani, Cannavaro na Bossou hao wote wanacheza kibabe na mikwara mingi ndani ya uwanja, hivyo kwa aina yao hiyo ya uchezaji inaweza kuwa tatizo kwake,” alisema Mgosi.

Post a Comment

 
Top