IMEBAINIKA kuwa Yanga haikufanya mazoezi ya pamoja ndani ya siku tatu kabla ya kuvaana na Ndanda jana Jumatano na kutoka nayo sare ya bila kufungana.
Katibu wa Yanga SC, Baraka Deusdedit amekiri kuwa wachezaji wa timu hiyo hawakufanya mazoezi siku tatu kabla ya mchezo na Ndanda kutokana na ratiba kubana.
Deusdedit alisema kwamba kilichotokea ni kocha Mholanzi Hans van der Pluijm aliwapa mapumziko wachezaji wikiendi (Jumamosi na Jumapili) na bahati mbaya Jumatatu kukawa na kikao na Mwenyekiti, Manji katika utaratibu wa kawaida wa klabu.
“Kwa hiyo kama kuna dhana hiyo ya timu kutoa sare jana kwa sababu ya kutofanya mazoezi siku tatu, benchi la Ufundi litasema katika taarifa yake,” alisema Baraka.
Pamoja na hayo, Baraka akalalamikia Yanga kupangiwa mechi nyingine ya Ligi Kuu Jumamosi dhidi ya Maji Maji, wakati jana wamecheza Mtwara.
“Sisi tumeondoka leo Mtwara, tutafika Dar es Salaam mchana na hatutafanya mazoezi leo. Kesho ni Ijumaa na keshokutwa Jumamosi tuna mechi nyingine, wakati Simba waliocheza jana Dar es Salaam wana mechi nyingine Jumapili,”alisema.
Hata hivyo baada ya sare hiyo benchi la ufundi la Yanga lililalamikia ubovu wa Uwanja wa Nangwanda Sijaona kuwa hauna viwango pamoja na wachezaji wake kuwa na uchovu.

Post a Comment

 
Top