OFISA Habari wa Simba, Haji Manara, juzi Jumatano alijikuta akidondosha machozi ya furaha baada ya baadhi ya wanachana wa Klabu ya Yanga kumkabidhi mchango wao kwa ajili ya matibabu ya tatizo la macho linalomkabili.

Manara anasumbuliwa na tatizo la jicho la kushoto ambapo limepoteza uwezo wa kuona huku lingine likiwa limepunguza uwezo wa kuona pia.

Wanachama wakiongozwa na Ofisa Habari wa Yanga, Jerry Muro walimkabidhi Manara shilingi 1,055,000 ambapo anatarajiwa kusafiri kwenda nje ya nchi kutibiwa wikiendi hii.

Akizungumza baada ya kupokea fedha hizo, Manara alisema: “Nawashukuru sana Yanga hususan ndugu yangu Jerry kwa msaada huu mlionipatia kwa ajili ya matibabu, hakika mmeonyesha kuwa utamaduni huu ndiyo unaotakiwa na hivyo ndivyo walivyokuwa wakiishi wazee wetu wa zamani.
Jerry muro na Hajji

“Soka siyo uadui kama baadhi ya watu wanavyodhani, nawashukuru sana kwa uamuzi wenu huo kwa sababu mmenipunguzia mzigo katika gharama za matibabu kwani zinazotakiwa ni zaidi ya dola 10,000 (shilingi milioni 20).”

Upande wa Muro alisema: “Tunakuombea kwa Mungu ili upone na urejee katika mapambano, tunakuomba siku utakayoondoka utuambie ili tukusindikize uwanja wa ndege lakini pia utakapokuwa unarudi nchini tuambie ili tuje tukupokee, wewe ni ndugu yetu na ni kaka yetu, tunakupenda kutoka rohoni.”

Post a Comment

 
Top