MATOKEO mabaya ya Yanga katika hatua
ya makundi ya Kombe la Shirikisho barani Afrika, yanalifikirisha benchi la
ufundi la timu hiyo hasa katika mpangilio wa kikosi kwa msimu ujao wa ligi na
michuano ya kimataifa.
Yanga juzi ilikubali kipigo cha mabao
3-1 kutoka kwa Madeama ya Ghana, ikiwa ni mchezo wa nne wa Kundi A la michuano
hiyo, huku ikiwa timu pekee kwenye kundi lake iliyopoteza mechi tatu na
kuambulia sare moja tu.
Mchezo wa juzi ulidhihirisha wazi
kwamba Yanga inahitaji kukitazama upya kikosi chake kuanzia aina ya wachezaji
wa kigeni ilionao hadi wale wa ndani hasa katika nafasi ya ulinzi na kiungo
mkabaji ambazo zinaonekana kupwaya mno.
Haja ya kukiangalia upya kikosi
kizima cha Yanga kwa ajili ya faida ya timu hiyo kwenye michuano ya kimataifa,
imeonekana baada ya mchezo dhidi ya Madeama ambapo kocha mkuu wa timu hiyo
Mholanzi, Hans Van der Pluijm, ameeleza masuala kadhaa ya msingi kwenye timu
hiyo.
“Inawezekana nina kikosi kizuri sana,
lakini kinafanya makosa ya kila mara ambayo yanaigharimu timu, sasa lazima
kuangalia upya kikosi chote, ni kweli hatuna kiungo mkabaji wa uhakika na hili
si tatizo la Yanga pekee lakini nadhani Tanzania nzima ukiangalia hakuna kiungo
wa kariba hiyo,” alisema kocha huyo.
Pluijm alisema kikosi chake
kimeonekana kuwa na upungufu kadhaa na kuahidi atafanya marekebisho makubwa
kuelekea michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika mwakani.
Pluijm alisema kadiri wanavyocheza
mechi hizo za kimataifa anabaini kwamba kuna jambo linahitajika kwenye timu
yake ndiyo maana anasisitiza usajili wa uhakika utakaoihakikishia Yanga nafasi
ya kuwa timu bora zaidi msimu ujao.
“Labda tuangalie namna tunavyosajili
sasa, ni kweli tuna kikosi kizuri lakini tujiulize upya ni kizuri kwa maana
ipi? Kwa ligi ya ndani au michuano ya kimataifa? Naamini timu yangu iko vizuri
lakini inapungukiwa vitu muhimu ambavyo sasa lazima tuvivalie njuga,” alisema.
Alisema safu ya ushambuliaji
inapoteza nafasi nyungi sana, anahitaji mtu mwenye kulijua lango vizuri licha
ya kwamba kuna Donald Ngoma, Obrey Chirwa, Amissi Tambwe, Malimi Busungu na
Matheo Anthony.
Pluijm alisema kuelekea katika
michuano mwakani, Yanga inahitaji aina ya mshambuliaji mwenye uwezo wa
kupambana na mabeki na pia kuwa na mshambuliaji mwenye shabaha ya kufunga mabao
na ambaye anaweza kubadilisha matokeo wakati wowote.
Alisema Yanga ina kikosi kipana
chenye wachezaji nyota, lakini kuelekea katika michuano ya kimataifa kinahitaji
kuwa na watu wa kazi wa kuleta matokeo mazuri.
“Kiungo mkabaji hili halina ubishi,
lazima nipate mtu wa kazi, mrefu na mwenye nguvu na nidhamu ya kucheza nafasi
hiyo, upande wa kulia pia kunahitajika kuongezwa nguvu. Na eneo la ulinzi la
kati nalo linahitaji maboresho kwa sasa hasa kuelekea michezo ya kimataifa
mwakani,” alisema.
Alisema ni lazima kikosi chake
kifanye usajili wa nguvu katika eneo la beki wa kushoto, mabeki wa kati na
kiungo mkabaji nafasi ambazo zimekuwa zikipwaya mara kadhaa hasa wanapokutana
na timu ngumu kwenye mechi za kimataifa.
Post a Comment