NA FARAJA MASINDE,
MIEZI michache nyuma, timu ya mpira wa kikapu ya Cleveland
Cavaliers ilifanikiwa kuweka historia kwenye fainali ya michuano ya ligi ya
kikapu ya Marekani, NBA, baada ya kuifunga Golden State Warriors kwa vikapu
93-89.
Hizi zilikuwa ni habari njema hata kwa rais wa taifa hilo,
Barack Obama, kufuatia ushindi huo ambao ulikuwa ni wa kwanza kwa Cavaliers
dhidi ya Warriors, ambao waliwafunga Cavaliers kwenye mchezo wa fainali ya
mwaka jana. Ilikuwa ni timu ya kwanza kufanikiwa kushinda taji hilo kutoka
kupoteza michezo mitatu ya awali na kushinda kwenye mchezo wake wa saba na
kutwaa taji la NBA.
Hata hivyo, ni lazima utambue kuwa nyuma ya mafanikio ya timu
hiyo kuna mtu anaitwa, LeBron James, 32.
“Nimekuwa na ndoto hii kwa zaidi ya miaka miwili toka nije
ili kuleta taji kwenye mji huu. Nilitoa kila kitu nilichokuwa nacho. Niliweka
moyo wangu, damu, jasho na machozi yangu kwenye mchezo huu,” hayo ni maneno ya
LeBron aliyoyatoa siku hiyo huku akilia kutokana na kutoamini ushindi ilioupata
timu yake.
LeBron alirejea kuichezea Cleveland mwaka 2014, baada ya
kutumia miaka minne akiwa na timu ya Miami Heat, ambapo pia akiwa na timu hiyo
alifanikiwa kutwaa nayo taji la NBA kwenye fainali.
LeBron aliiongoza timu yake kupata taji la mwaka huu baada ya
kufunga alama nyingi zaidi kwenye mchezo mmoja, ambapo siku ya fainali ya
mwisho alifunga alama 27, huku akipata ribaundi 11 na kusaidia wenzake kufunga
mara 11, ushindi ambao pia ulimfanya atajwe kama mchezaji mwenye thamani zaidi
kwenye mchezo wa fainali, tuzo inayofahamika kama MVP.
Ni kweli kuwa kwasasa unapotaja mafanikio ya NBA huwezi
kuliacha jina hili, kwani mafanikio yake si tu kwamba yalikuja mara baada ya
kuisaidia Miami Heat kutwaa uchampioni wa NBA mwaka 2012 na 2013, bali tangu
akiwa mdogo kabla ya kujiunga na Cleveland Calalier.
LeBron, ambaye ni mzaliwa wa Anron, Ohio Marekani, aliyeweka
historia mwaka huu katika Ligi Kuu ya Kikapu nchini Marekani na kubaki kwenye
vichwa na wafuatiliaji wa NBA kipaji chake kilianza kuonekana tangu akiwa na
umri mdogo.
Historia
LeBron Raymone James alizaliwa Desemba 30, 1984, kipaji chake
hicho kiligunduliwa katika shule za St. Vincent na St. Mary, ambapo
alishawishiwa kujiunga na timu ya mpira wa kikapu mwaka 1990.
Mara baada ya kujiunga na timu hiyo, milango yake ilianzia
hapo kufunguka na hii ilikuwa ni baada ya kuwa na wastani wa pointi 18 kila
mchezo, ambapo aliisaidia timu yake kumaliza daraja la tatu ikiwa na ushindi wa
pointi 25.
Kuanzia hapo ndipo umaarufu wa LeBron ulipoanza kusambaa
duniani kote ambapo alianza pia kupokea tuzo mbalimbali za heshima kutokana na
kufanya vizuri kwenye kikapu.
Miaka michache baadaye alijiunga na shule ya Sophomore ambapo
akiwa hapo, alichaguliwa na gazeti la USA today kuwa miongoni mwa waliokuwa
wakiunda kikosi cha kwanza cha Marekani kwenye mchezo wa kikapu.
Mara baada ya kuhitimu masomo, James alijiunga na timu ya
wakubwa shuleni hapo ambapo kuanzia hapo alikuwa na wastani wa pointi 31.6 kila
mchezo, hali iliyosaidia timu yake kufanya vyema kwenye msimu huo hali
iliyosaidia kuingia kwenye orodha ya timu bora za taifa.
Hiyo ilikuwa ni mara baada ya yeye kushinda pointi 2,657 kwa
miaka minne aliyokuwa na timu hizo za St Vincent na St Mary.
Kutokana na hamasa kubwa aliyokuwa nayo, LeBron alitajwa kuwa
mchezaji bora wa kikapu kwa mwaka 2003 wa ligi ya ndogo ya NBA.
Ni mafanikio hayo ndiyo yaliyochochea timu ya Cleveland
Cavaliers kuingia naye mkataba kama mshambuliaji kijana ambaye aliisaidia timu hiyo kumaliza katika nafasi
ya pili ikilinganishwa na mwaka mmoja nyuma timu hiyo iliposhika nafasi ya nane
kwenye ukanda wa Mashariki.
Maisha binafsi
Nje ya NBA, LeBron amekuwa akifanya kazi kwa ajili ya
kusaidia wengine ambapo alianzisha mfuko
wa LeBron James Family mwaka 2004, mama yake anaitwa, Gloria, ambaye awamekuwa
wakifanya naye kazi ya kusaidia watoto yatima na familia zenye mzazi mmoja
asiyejiweza kupata mahitaji.
Miongoni mwa mambo ambayo yanafanywa na mfuko huo pia,
ilikuwa ni kusaidia kuandaa mikakati mbalimbali ya kuinua uchumi kwenye maeneo
yaliyoanguka kiuchumi.
Mke wake anaitwa, Savannah Brinson, ambaye wako pamoja tangu
wakiwa shule na wamebahatika kupata watoto watatu, LeBron James Jr, Bryce
Maximus James, Zhuri James. Baba yake ambaye ni Anthony McClelland,
alishafariki siku nyingi.
Usafiri
Anamiliki gari aina ya Lamborghini Aventador, ambalo alinunua
mwaka jana ambapo taarifa za chini chini zilieleza kuwa gari hilo pamoja na
viatu vyake vya Nike vinagharimu dola
670,000 ambapo gharama hizi zote zililipwa na Kampuni ya Nike.
Mjengo
LeBron ambaye anatajwa kama mtu mwenye jicho la kibiashara
zaidi, anamiliki nyumba zaidi ya mbili ikiwamo ile aliyotumia kiasi cha dola
milioni 20.98 kwa mujibu wa jarida la ‘LA Times’ ambayo iko Miami, iliyo na
bwawa la kuogelea ndani yake, baa, sehemu ya kuegesha magari, vyumba sita vya
kulala, vyoo nane, studio ya muziki, Casino, saluni na vingine.
Mkwanja
LeBron ambaye alianza kucheza kikapu akiwa na umri wa miaka 9
peke yake, anatajwa kama moja ya wachezaji wa NBA wanaomiliki fedha nyingi
zaidi ambapo anakadiriwa kuwa na utajiri
wa zaidi ya dola milioni 300.
Mwaka 2014, alivuna kiasi cha dola milioni 75 kutoka NBA hiyo
ikitokana na mshahara wake ambapo alikuwa akikunja kiasi cha dola milioni 19.3.
Kama hujui kwa mwaka huo alikuwa akishikilia nafasi ya tatu
kwa wanamichezo wanaolipwa fedha nyingi zaidi duniani, nyuma ya Cristiano
Ronaldo (dola milioni 80) na Floyd Mayweather Jr (dola milioni 105) ambaye
alikuwa akishika nafasi ya kwanza. Achilia mbali mikataba ya Nike, Apple,
Microsoft, Samsung, Dre, state farm na Dunkin Donuts.
Namna teknolojia inavyokuza jina lake
Kwa ulimwengu huu wa leo eneo hili la teknolojia kamwe huwezi
kulikimbia kama kweli unahitaji mafanikio ndivyo ilivyotokea pia kwa LeBron
James.
Kurejea kwake Cleveland kuliamsha nguvu mpya na hapo ndipo
lilipokuja jina la Mfalme LeBron. Hapa ni baada ya kutumia vyema eneo la teknolojia
katika kumweka karibu na mashabiki wake
ambapo alikuwa akisambaza picha za jezi zake kwenye mitandao mbalimbali
hali iliyochangia umaarufu wa jina lake ikilinganishwa na kipindi cha miaka
mitano nyuma.
Baada ya kuona mafanikio hayo, mtandao wa kijamii wa Youtube
uliziweka video zake kwenye mtandao wao huo
kama heshima kutokana na kipaji chake na hivyo kumsogeza kwenye mikataba
minono na makampuni makubwa kama Nike na mengine.
Kwani wapo waliolazimika kumtungia nyimbo maalumu ukiwamo ule
wa Lebrons national, hili ni jambo ambalo hata LeBron mwenyewe anakiri kuwa
teknolojia ndiyo chanzo cha yote haya.
Kwani imemwongezea mashabiki lukuki kila kona ya dunia na
hata kuwavuta wale ambao hawakuwa na mapenzi
na mchezo huo wa kikapu kuanza kufuatilia kwa makini.
Kama kawaida kila mmoja kwa wakati wake alianza kutuma picha
za umbo lake huku akijifananisha na LeBron.
Pointi ya msingi hapa ni kuwa
anatumia mitandao ya kijamii na teknolojia nyingine kukuza jina lake, vikiwamo
viatu aina ya Lebron 12 alivyotengenezewa na Kampuni ya Nike kwa ajili ya
kikapu, viatu ambavyo viliingia sokoni Oktoba 30 mwaka jana.
Namba ya mwandishi 0653045474.
Post a Comment