WAKATI beki wa kulia wa Yanga, Hassan Kessy
akiendelea kufanya mazoezi na kikosi cha timu hiyo bila ya kujua ni siku gani
ataitumikia, hali hiyo imeonekana kumuumiza roho na kujikuta akisema kuwa
endapo sakata lake na Simba litaendelea hivyo basi yupo tayari kukaa nje ya
uwanja kwa msimu mzima.
Kessy ambaye alijiunga na Yanga hivi
karibuni anashindwa kuitumikia timu hiyo kutokana na kile kinachodaiwa uongozi
wa klabu hiyo haukuzingatia taratibu za usajili wakati ulipokuwa ukimsajili
kutoka Simba.
Kutokana na hali hiyo uongozi wa
Simba unataka Yanga ilipe Sh milioni 126, ili Kessy aweze kuitumikia vinginevyo
hataitumikia klabu hiyo, jambo ambalo lilimfanya Kessy kwenda kuomba msaada kwa
Chama cha Wachezaji wa Soka Tanzania (Sputanza), ili waweze kumsaidia
kuhakikisha anapata kibali kutoka TFF, kitakachomwezesha kuitumikia timu hiyo
mpya.
Kessy alisema mpaka sasa hakuna
kilichofikiwa na kama hali hiyo itaendelea kama ilivyo sasa basi yupo tayari
kukaa nje ya uwanja kwa msimu mzima.
“Suala langu bado linaendelea na
mpaka sasa sijapata jibu lolote kutoka Sputanza hata hivyo kama itaendelea hivi
basi nitasubiri mpaka litakapomalizika hata kama itakuwa ni kukaa nje msimu
mzima mimi nitakaa.
“Kuhusu kiwango changu kushuka
naamini hakitashuka kwa sababu nipo katika timu nzuri. Lakini pia nipo chini ya kocha mzuri ambapo nitakuwa
nafanya mazoezi kwa nguvu zangu zote mpaka hapo suala hili litakapomalizika,”
alisema Kessy.
Post a Comment