SIKU mbili tangu kikosi cha Simba kilipoisurubu Polisi Morogoro mabao 6-0, kocha mkuu
wa timu hiyo, Mcameroon, Joseph Omog, amedai kuwa kikosi chake hicho hivi sasa
kipo tayari kwa michuano ya Ligi Kuu Bara.
Mchezo huo wa kirafiki ulifanyika katika Uwanja wa Chuo cha
Biblia kilichopo Bigwa mkoani Morogoro ambako timu hiyo imepiga kambi yake ya
kujiandaa na ligi kuu inayotarajiwa kuanza kutimua vumbi Agosti 20, mwaka huu.
Omog alisema kuwa kiwango kilichoonyeshwa na wachezaji wake
katika mchezo huo ni cha hali ya juu hivyo hata kama ligi kuu itaanza leo basi
ana uhakika kuwa watafanya vizuri.
“Kwa sasa kikosi changu kipo vizuri na tayari kabisa kwa
michuano ya ligi kuu kutokana na kiwango cha juu kilichoonyeshwa na wachezaji
katika mechi yetu ya kirafiki dhidi ya Polisi Morogoro.
“Kila mchezaji aliyepata nafasi ya kucheza alionyesha kiwango
kikubwa hali ambayo ilinifanya niamini hivyo,” alisema Omog.
“Kuhusu hatima ya wachezaji wa kimataifa wanaoendelea kujifua
na kikosi chake, Omog alisema: “Wanafanya vizuri lakini kila kitu kitajulikana
hivi karibuni nani atabaki na nani ataondoka, hivyo tuwe na subira.”
Omog alikabidhiwa mikoba ya kukinoa kikosi hicho hivi
karibuni ambapo hivi sasa yupo katika harakati za kukisuka upya akisaidiana na
Mganda, Jackson Mayanja ili kiweze kurudisha heshima yake iliyopotea kwa muda
mrefu bila ya kushiriki michuano ya kimataifa lakini pia kunyakua ubingwa wa
ligi hiyo.
Post a Comment