MSHAMBULIAJI wa Yanga,
Mrundi, Amissi Tambwe, amewataka wapinzani wao Simba waendelee kuchonga, lakini
watawatambua mara Ligi Kuu Bara itakapoanza.
Hiyo ni baada ya wapinzani
wao hao kuwapiga vijembe kutokana na matokeo mabaya waliyoyapata kwenye mechi
tatu za mwanzoni kwenye Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya MO Bejaia, TP
Mazembe ambazo zote walifungwa bao 1-0 kabla ya kutoka sare na Medeama 1-1.
Timu hiyo, jana jioni
ilitarajiwa kurudiana na Medeama nyumbani kwao Ghana baada ya sare hiyo kabla
ya kuvaana na MO Bejaia kisha TP Mazembe.
Tambwe alisema hasira zao
zote wanazihamishia kwenye ligi kuu iliyopangwa kuanza kutimua vumbi Agosti 20,
mwaka huu na kikubwa walichopanga ni kuendeleza ubabe wa kulitetea taji hilo la
ubingwa wanalolishikilia.
Tambwe alisema, wanatumia
michuano hiyo kama maandalizi ya ligi kuu, licha ya kuwa na nafasi ya kufuzu
Nusu Fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika kama watashinda michezo mitatu
waliyoibakiza dhidi ya Medeama (jana), MO Bejaia na TP Mazembe.
Aliongeza kuwa, hao wapinzani
wanaofurahia matokeo mabaya wanayoyapata wajiandae kutokana na maandalizi yao
ya muda mrefu waliyoyafanya.
“Siku zote timu pinzani moja
inapofanya vibaya, basi wapinzani wao lazima wafurahie, hivyo tunajua wapinzani
wetu hivi sasa wanafurahi na kuongea maneno mengi ya kashfa juu yetu, lakini
sisi tuwaambie tutaonana kwenye ligi.
“Sisi hatujapumzika kabisa
tangu msimu uliopita ulipomalizika na badala yake tulikuwa tukishiriki michuano
ya kimataifa, hivyo utaona jinsi gani timu ilivyokaa pamoja muda mrefu, tayari
wachezaji wapya na wa zamani tumeshazoeana.
“Hivyo, kazi wanayo wao
wanaoanza ‘Pre Season’ ambao watatukuta sisi tupo vizuri na tayari kwa ajili ya
ligi kuu tukitaka kuutetea ubingwa wetu,” alisema Tambwe aliyemaliza ligi kuu
akiwa mfungaji bora akipachika mabao 21.
Post a Comment