KIKOSI cha Yanga kinatarajia kuondoka nchini keshokutwa
Ijumaa kuwafuata Medeama ya Ghana tayari kwa mchezo wa marudiano wa kuwania
Kombe la Shirikisho Afrika.
Hata hivyo, katika safari hiyo beki wa kulia wa Yanga
aliyejiunga na timu hiyo hivi karibuni akitokea Simba, Hassan Kessy, anaweza
kuikosa mechi hiyo kutokana na sakata lake la usajili linaloendelea hivi sasa
kati yake na Simba.
Habari za kuaminika kutoka Yanga zimedai kuwa maandalizi kwa
ajili ya safari hiyo yanaendelea lakini pia kocha mkuu wa timu hiyo, Mholanzi,
Hans van Der Pluijm yupo katika maandalizi makali kwa ajili ya mchezo huo
unaotarajiwa kuwa na ushindani mkubwa siku ya Jumanne ijayo, Julai 26, mwaka
huu.
“Tupo katika maandalizi makali kwa ajili ya mechi yetu ya
marudiano na Medeama itakayofanyika Jumanne ijayo ili kuhakikisha tunafanya
vizuri kwani nafasi tuliyopo hivi sasa inatunyima usingizi.
“Mungu akipenda kama mambo yatakuwa sawa tutaondoka Ijumaa
hii ila wachezaji ambao hawatacheza mechi hiyo kutokana na kuwa na adhabu
mbalimbali na wale ambao hawajapata kibali cha kuitumikia Yanga basi tunaweza
kuwaacha lakini tunasubiria mapendekezo ya kocha,” alisema mtoa habari huyo.
Alipoulizwa kuhusiana na suala hilo Katibu Mkuu wa Yanga,
Baraka Deustedit hakuwa tayari kulizungumzia zaidi ya kudai kuwa: “Muda ukifika
kila kitu kitajulikana.”
Yanga itakwenda nchini Ghana ikiwa na kumbukumbu ya kutoshana
nguvu ya kufungana bao 1-1 na Medeama Jumamosi iliyopita kwenye Uwanja wa Taifa
jijini Dar es Salaam.
Yanga kwa sasa inashika mkia kwenye Kundi A ikiwa na pointi
moja huku TP Mazembe wakiwa kinara na pointi saba, wakifuatiwa na MO Bejaia
wenye pointi tano.
Post a Comment