RASMI uongozi wa Simba umethibitisha kufuzu kwa kiungo wao, Jonas Mkude aliyekwenda kufanya majaribio katika Klabu ya Mpumalanga inayoshiriki Ligi Kuu ya Afrika Kusini.

Kiungo huyo, alikuwepo kwenye majaribio hayo kwa muda wa wiki mbili mara baada ya kuitwa kufanya majaribio ya kucheza soka la kulipwa nchini humo ikiwa ni mara yake ya pili kwenda kwenye majaribio nchini humo ambapo awali alikwenda katika timu ya Bidvest lakini hakufanikiwa.

Rais wa Simba, Evans Aveva, ameliambia gazeti hili kuwa Mkude amefuzu majaribio lakini kilichokwamisha ni maslahi ambayo alitakiwa kupewa.

Aveva, amesema wao walijiridhisha kumuachia Mkude lakini mchezaji mwenyewe ndiye aliyekataa kutokana na maslahi madogo ya mshahara na fedha za usajili ambazo alitakiwa kupewa.


“Mpumalanga imeshindwa yenyewe kutoa ofa nzuri itakayomshawishi Mkude na uongozi, hiyo ni baada ya kutangaza kutoa ofa ndogo ambayo mchezaji mwenyewe hakuridhishwa nayo kabla ya kuomba kurejea nchini.

“Kama uongozi tulitoa nafasi ya mchezaji mwenyewe kuridhia kwenda huko kwa ofa ndogo waliyoitoa, lakini mwenyewe akakataa, tunaheshimu maamuzi yake na kumuacha kurejea kwenye timu yake ya Simba.

“Ilikuwa ni ngumu Mkude kucheza soka huko kwa mshahara wa dola 1,500 (Sh milioni 3), kama unavyojua kuna kukatwa kodi huko, hivyo ameona ni bora akaendelea kulipwa mshahara anaoupata hapa wa shilingi milioni mbili,” alisema Aveva.

Post a Comment

 
Top