KOCHA Bora wa msimu uliopita wa Ligi Kuu Bara, Hans van Der Pluijm wa Yanga,
amesema wataishangaza Medeama SC kwa kuifunga nyumbani kwao Ghana Jumanne ijayo
kwenye mechi ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Pluijm, raia wa
Uholanzi, alienda mbali kwa kusema, haoni sababu ya wao kushindwa kupata
matokeo mazuri nchini Ghana wakati timu yake itakaporudiana na Medeama.
Mechi hiyo ya marudiano
ya Kundi A ikiwa na kumbukumbu ya kutoka sare ya bao 1-1 hapa nchini.
Pluijm alisema kupoteza
pointi mbili mechi ya nyumbani siyo sababu ya timu yake kushindwa kuifunga
Medeama wakiwa kwenye uwanja wao wa nyumbani.
Pluijm alisema, siyo
kazi rahisi kwao kuwafunga Medeama nyumbani kwao, lakini watapambana kwa pamoja
kuanzia benchi la ufundi, viongozi na wachezaji kuhakikisha wanafanikisha hilo.
Aliongeza kuwa, tayari
ameona mbinu na mifumo wanayotumia Medeama, hivyo amekiboresha kikosi chake ili
kutimiza malengo, licha ya ugeni walionao kwenye michuano hiyo kwa hatua
waliyofikia.
“Kadiri siku zinavyoenda
benchi langu la ufundi na wachezaji kwa pamoja tunazidi kupata uzoefu wa
michuano hii katika hatua hii tuliyoifikia ya mashindano haya.
“Hivyo, tunakwenda
kurudiana na Medeama tukiwa tumepata uzoefu wa michuano hii katika nafasi hii
ya hatua ya makundi, hivyo tutawavaa Medeama tofauti na watakavyotarajia, licha
ya kumkosa Bossou (Vincent) mwenye adhabu ya kadi mbili za njano, nitamtumia
Cannavaro (Nadir Haroub),” alisema Pluijm.
Kwa upande wake, nahodha
wa Yanga, Cannavaro alisema: “Wanayanga na Watanzania wote wanatakiwa
kutuombea, tunakwenda kupambana na timu bora siyo nyepesi.”
Post a Comment