BAADA ya kukabidhiwa Tuzo ya Ufungaji Bora wa Ligi Kuu
Bara 2015/2016, straika wa Yanga, Amissi Tambwe amefunguka kuwa siri kubwa ya
mafanikio yake uwanjani ni kujituma na kutumia akili kufanya maamuzi na kudai
kuwa hana imani na masuala ya kishirikina.
Tambwe alikabidhiwa tuzo hiyo baada ya kufunga mabao 21 na
kuonyesha kuwa ana uwezo mkubwa wa kufunga kwa kuwa amekuwa akifanya hivyo
tangu alipokuwa akiichezea Simba.
“Mafanikio yangu wala hakuna juju (ushirikina), siri
kubwa ni kujituma kwangu na kuwazidi akili mabeki wengi hawa wa kwenye ligi
kuu.
“Unajua mabeki wengi wa hapa Tanzania wanatumia nguvu
nyingi kunikaba, pia wananipania sana, hivyo mimi ninachofanya ni kucheza kwa
ujanja na kutumia akili nyingi.
“Mbinu nyingine ninazozitumia ni kucheza na eneo la ndani
ya boksi la timu pinzani kwa ajili ya kusubiria pasi za mwisho, krosi na kona
kutoka kwa mawinga na mabeki wetu wa pembeni ambao ni wazuri kwa kupiga mipira
hiyo,” alisema Tambwe.
Kuhusu kutong’ara kimataifa, Tambwe alisema huko
anakutana na mabeki wengi wanaotumia akili nyingi na uzoefu wa kukaba, hali
inayosababisha apate ugumu wa kufunga mabao.
Aidha, aliongeza kuwa kuongezeka kwa majukumu uwanjani
kama anavyoagizwa na kocha wake, Hans van Der Pluijm kucheza namba 10 tofauti
na mwanzoni alikuwa akicheza namba 9, kumesababisha kasi yake ya kufunga mabao
kupungua.
CHANZO: Championi
Post a Comment