MCHEZAJI
kiraka wa Yanga, Mnyarwanda, Mbuyu Twite, ameonyesha kuwa popote uwanjani
anacheza kwa kiwango kilekile, baada ya kuchezeshwa nafasi tatu tofauti kwenye
mechi za timu hiyo, hivi karibuni.
Twite
ambaye hivi karibuni jina lake lilikuwa kwenye hatari ya kukatwa katika usajili
wa timu hiyo, mpaka sasa ameshacheza mechi tatu za Yanga za kimataifa kwa
dakika zote tisini mfululizo ambazo ni sawa na dakika 270.
Katika
mchezo dhidi ya MO Bejaia ya Algeria, Twite alichezeshwa beki wa kulia baada ya
Juma Abdul kuwa majeruhi, huku Hassan Kessy akizuiwa kucheza kutokana na
uhamisho wake kutoka Simba kutokamilika.
Mchezo
uliofuata wa michuano hiyo dhidi ya TP Mazembe, Twite alichezeshwa beki wa
kushoto baada ya Oscar Joshua na Haji Mwinyi kuwa majeruhi.
Twite
alidhihirisha kwamba yeye ni mtu muhimu kikosini hapo juzi Jumamosi walipocheza
dhidi ya Medeama ambapo alitia fora kwa kucheza nafasi mbili tofauti.
Mnyarwanda
huyo mwenye asili ya DR Congo, alianza kama kiungo mkabaji ambapo alicheza kwa
dakika 78, lakini mara baada ya Oscar Joshua aliyekuwa akicheza beki wa kushoto
kutolewa na nafasi yake kuchukuliwa na Haruna Niyonzima, Twite akacheza beki
hiyo ya kushoto.
Kocha
wa Yanga, Hans van Der Pluijm,
amemmwagia sifa mchezaji huyo akisema: “Kila ninapompatia majukumu ya kufanya
uwanjani amekuwa akiyafanya kwa umakini mkubwa bila ya kuniangusha, hakika
napongeza kwa hilo na nitaendelea kumtumia katika mechi zetu zijazo.”
Kwa upande wake Twite alisema: “Hicho ni
kipaji nilichopewa na Mungu, hivyo ninamshukuru Mungu kwa hilo, lakini pia
najisikia faraja kwa kufanikiwa kuandika rekodi hiyo nikiwa na Yanga.”
Post a Comment