SIKU za nyuma kidogo hali ya uoga iliitwa
kuchachawa, sasa Medeama SC ya Ghana imechachawa na kuiomba Bodi ya Ligi Kuu ya
Ghana kuahirisha mechi yao moja ya Ligi Kuu ili ijiandae kuivaa Yanga.
Baada
ya sare ya bao 1-1, wikiendi iliyopita jijini Dar es Salaam, Medeama itarudiana
na Yanga, Jumanne ijayo jijini Accra, Ghana katika mchezo huo wa Kundi A la
Kombe la Shirikisho Afrika.
Kutokana
na umuhimu wa mchezo huo, Medeama imeomba na kuruhusiwa kutocheza mechi yake ya
ligi kuu iliyopaswa kuchezwa leo Jumamosi dhidi ya Wa All Stars.
Kwa
mujibu wa habari kutoka Ghana, Medeama ndiyo waliopeleka maombi ya mchezo huo
usogezwe mbele ili waweze kujiandaa vizuri chini ya Kocha Pride Owusu.
Mara
baada ya Medeama kukabidhi barua ya maombi hayo, bodi ya Ligi Kuu ya Ghana
ilikubali na kuipa nafasi zaidi timu hiyo kujiandaa na mechi dhidi ya Yanga,
pia kuwapa wachezaji muda wa kutosha wa mapumziko.
Katika
ligi kuu, Medeama ipo nafasi ya tatu ikiwa na pointi 33 katika mechi 19
ilizocheza na inaonekana inaweza kufanya vizuri hivyo kuwa na matumaini ya
kushiriki tena Michuano ya Shirikisho la Soka Afrika (Caf) msimu ujao.
Katika
Kundi A, Medeama inashika nafasi ya tatu ikiwa na pointi mbili huku Yanga ikiwa
mkiani na pointi moja wakati TP Mazembe ikiwa kileleni na pointi saba na MO
Bejaia ni ya pili na pointi tano. Timu zote zimecheza mechi tatu.
Post a Comment