Cristiano Ronaldo aliamua kurejea Madeira mji aliokua, akitokea kwenye mapumziko ya muda katika kipindi hiki cha majira ya joto barani Ulaya.

Haikuwa kwa sababu nyingine bali ni kuzindua hoteli yake ya kifahari inayokwenda kwa jina la Pestana CR7 hotel.

Ronaldo kwa sasa ni mmiliki wa hoteli hiyo yenye vyumba 46, alisimama kwenye makumbusho yake na kujibu maswali kadhaa ya wanahabari.

Katika safari yake ya Madeira, Cristiano Ronaldo amejibu maswali mengi ya waandishi wa habari ikiwa ni pamoja na gazeti maarufu linalojulikana kwa jina la Marca.

Ronaldo amethibisha kwamba, hatocheza kwenye mchezo wa Super Cup kati ya Real Madrid dhidi ya Sevilla: “Nimetolewa kabisa kwenye mipango ya mchezo wa UEFA Super Cup utakaochezwa tarehe 9, kwasababu mimi nitaanza majukumu (na Real Madrid) tarehe 10.”

Nyota huyo wa Ureno pia akathibitisha kwamba anataka kubaki Real Madrid: “Nimezungumza na Rais kwa njia ya simu na nikirejea Madrid tutazungumza. Kiuhalisia, kuongeza mkataba ni kitu ambacho nakihitaji.”

Cha kushangaza ni kwamba, hafikirii sana kuhusu kushinda tuzo ya Ballon d’Or: “Ballon d’Or haipo mikononi mwangu lakini ninakiri kwamba nipo katika nafasi nzuri ukichukulia nimefanikiwa kushinda ubingwa wa Uefa Champions League na ubingwa wa mataifa ya Ulaya.”


“Msimu huu umekuwa bora kwenye maisha yangu ya soka, nimeshinda mataji mawili makubwa nikiwa na klabu yangu pamoja na nchi yangu kwahiyo lilikuwa ni jambo la kipekee…tuzo binafsi zinatwaliwa bila kutarajia, sifikirii sana kuhusu kushinda Ballon d’Or.”

Baada ya Ronaldo kupata majeraha kwenye mchezo wa fainali ya Euro 2016, anatarajiwa kurejea uwanjani kwa ajili ya msimu wa 2016/2017 mara baada ya mapumziko aliyopewa kwa ajili ya timu ya taifa kumalizika.


Ronaldo alizungumzia pia jeraha la goti alilopata kwenye fainali ya Euro: “Naendelea vizuri, nataka nipone vizuri na natarajia kurejea uwanjani mapema kadri iwezekanavyo.”

Post a Comment

 
Top