UMEBAKI muda mchache tu kabla ya sintofahamu ya mfanyabiashara maarufu, Mohammed Dewji (Mo), kukabidhiwa au kutokabidhiwa kuwekwa wazi baada ya mkutano mkuu wa klabu ya Simba ya jijini Dar es Salaam kufanyika Jumapili.

Wanachama wa klabu ya Simba wanatarajia kufanya mkutano wao mkuu Jumapili ya Mei 31, ambapo licha ya mambo mengi kutarajiwa kujadiliwa, suala la Mo kupewa timu linatarajiwa kutikisa.

Mo alitangaza kutaka kununua hisa zinazofikia asilimia (51%) ambapo angewekeza kiasi cha shilingi milioni 20 na baada ya kauli hiyo yaliibuka makundi mawili, moja likiunga mkono bilionea huyo apewe timu na lingine likionyesha wasiwasi.

Hata hivyo, kundi kubwa ndilo ambalo limekuwa likionyesha kumuunga mkono mfanyabiashara huyo apewe timu kwa madai kuwa ataisaidia klabu hiyo hasa kuwalipa mishahara wachezaji na benchi la ufundi na pia kufanya usajili wenye tija.

Moja ya sababu zinazowafanya mashabiki hao walio wengi kumuunga mkono Mo, ni kutokana na timu hiyo kukosa ubingwa kwa misimu minne mfululizo na mara kadhaa baadhi ya wachezaji wakilalamika kucheleweshewa mishahara yao.

Licha ya kwamba Mo alisema anaitaka Simba na hata kufikia kipindi akawapa muda wawe wamempa jibu, lakini mara kadhaa viongozi wa Wekundu hao wa Msimbazi walinukuliwa wakisema mfanyabiashara huyo hakufika mezani kwao kulizungumzia suala hilo.

Tangu Mo kutangaza kutaka kuwekeza katika klabu hiyo hapajakuwa na mkutano wowote na sasa jambo hilo linatarajiwa kuibuka upya mwishoni mwa wiki hii kwenye mkutano huo kwani baadhi ya mashabiki wamepania kupata jibu.

Wakati mkutano huo ukitarajiwa kuvuta hisia za wengi hasa juu ya jambo hilo, DIMBA Jumatano lilifanya mahojiano na baadhi ya viongozi wa matawi ya Simba juu ya mfanyabiashara huyo kuachiwa timu ama la.

Mwenyekiti wa Nyayo za Simba Mabibo, Ramadhani Pazi, alisema huu ni muda mwafaka Mo kukabidhiwa timu kwani mashabiki wanachokitaka ni furaha na kwa sasa duniani kote timu zimekuwa zikipata sapoti kubwa kutoka kwa wafanyabiashara.

“Mimi nimekuwa Simba tangu wakati huo ikiitwa Sunderland mpaka sasa bado nipo, kwa mawazo yangu huu ni muda mwafaka timu kukabidhiwa kwa mtu yeyote ambaye anaweza kuifanyia makubwa.

“Duniani kote tumeshuhudia hata zile timu kubwa zikipata sapoti kutoka kwa wafanyabiashara kama Dewji sasa ikiwa amekidhi vigezo na apewe hii timu, mimi sioni shida,” alisema kauli ambayo pia ilikuwa sawa na ile ya Katibu Mkuu wa tawi la Ngome Kongwe Tabata.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa tawi la Vuvuzela, Hamis Mkoma, alisema kwa sasa suala la Mo linatakiwa liwekwe kando kwanza mpaka pale wanachama watakapopewa elimu ya kutosha huku Katibu Mkuu wa tawi la Ubungo Terminal (UBT), Jastine Mwakitalima, akisema hapingani na wazo la Mo kupewa timu ila angalau angeonyesha moyo wa kutoa fedha wakati timu hiyo ilipokuwa katika hali ngumu ili kuthibitisha kuwa ana mapenzi ya dhati.

Post a Comment

 
Top