MSAFARA wa
wachezaji 21 wa Yanga, asubuhi ya kesho Jumamosi utaondoka kuelekea nchini
Ghana kwa ajili ya kukipiga na Medeama ya nchini humo huku wakiwaacha mabeki wao,
Hassan Kessy na Mtogo, Vincent Bossou.
Yanga itarudiana
na Medeama katika mechi ya Kombe la Shirikisho Afrika baada kutoka sare ya
kufungana bao 1-1 mchezo uliopigwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam,
Julai 16, mwaka huu.
Chini ya Kocha Mholanzi,
Hans van Der Pluijm, Yanga inatakiwa kushinda kwenye mchezo huo ili kujiweka
katika mazingira mazuri ya kufuzu kucheza Nusu Fainali ya michuano hiyo,
kinyume na hapo hali ya mambo inaweza kuwa mbaya na yawezekana wakawa wamefuta
ndoto za kusonga mbele.
Meneja wa Yanga,
Hafidh Saleh, amesema msafara wao unatarajiwa kuwa na watu 30, kati ya hao,
wachezaji ni 21 na viongozi tisa.
Amesema msafara
huo unatarajiwa kuondoka saa moja asubuhi kwenye Uwanja wa Ndege wa Julius
Nyerere (JNIA) wa jijini Dar kwa Shirika la Ndege la Kenya Airways (KQ).
Kuhusu Kessy, meneja
huyo amesema amebaki kwa kuwa hakuna mipango ya kumtumia kwa kuwa bado suala
lake la usajili ni kikwazo.
Kuhusu Bossou
hatakwenda kwa kuwa anatumikia adhabu ya kadi mbili za njano zitakazomkosesha mechi
hiyo. Kiungo wa timu hiyo, Deus Kaseke naye hatakwenda kwa kuwa Pluijm
ameshauri abaki kwa ajili ya kupumzika, licha ya kupona majeraha ya mwili
aliyoyapata kwenye ajali ya pikipiki, pia Geofrey Mwashiuya naye atabaki kwa
kuwa ana majeraha ya goti.
"Kessy bado
hajathibitishwa kuichezea Yanga kutokana na lile sakata lake na Simba,” alisema
meneja huyo.
Akizungumzia
suala hilo la kuachwa, Kessy alisema: “Sina jinsi, ndiyo hivyo imeshatokea,
nipo tu kambini kwa sasa, nasubiri wakiondoka mimi itabidi nirudi nyumbani
kuwasubiri wenzangu, lakini itabidi nilisimamie mimi mwenyewe wakati wenzangu
watakapokuwa Ghana. Inaniuma sana na ninasikitishwa na hali ya mambo
inavyoendelea.”
Wachezaji
watakaosafiri na timu ni Deogratius Munish 'Dida', Ally Mustapha 'Barthez',
Beno Kakolanya, Juma Abdul, Haji Mwinyi, Oscar Joshua, Mbuyu Twite, Nadir
Haroub 'Cannavaro', Kelvin Yondani, Pato Ngonyani.
Wengine ni Said
Juma 'Makapu', Andrew Vincent 'Dante', Thabani Kamusoko, Haruna Niyonzima,
Simon Msuva, Juma Mahadhi, Obrey Chirwa, Malimi Busungu, Amissi Tambwe, Donald
Ngoma na Anthony Matheo.
Post a Comment