NAHODHA wa Yanga, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, ameogopa na kusema msimu ujao
wa Ligi Kuu Bara unaweza kuwa mgumu kwao hata kutetea ubingwa kwani wana uchovu
wa kucheza mechi nyingi mfululizo.
Cannavaro
amesema hayo wakati Yanga ikiwa bado kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho
Afrika hatua ya makundi.
Tofauti
na timu nyingine za ligi kuu ambazo zilipumzika baada ya ligi hiyo kumalizika
Mei, mwaka huu, Yanga yenyewe iliendelea na mechi za Kombe la Shirikisho na
itacheza hadi Agosti 24, mwaka huu.
Yanga
inatarajiwa kumaliza mechi zake za Kundi A za Kombe la Shirikisho kati ya
Agosti 23 na 24, mwaka huu wakati msimu ujao wa ligi kuu ukianza Agosti 20,
yaani siku tatu au nne nyuma yake.
Cannavaro
alisema msimu uliopita walipata muda wa kupumzika na wakatetea vizuri ubingwa wa
ligi kuu, lakini safari hii hawajapumzika na mambo yanaweza kuwa magumu.
“Tangu
ligi imalizike hatujapumzika, halafu ukiangalia msimu mpya unatarajia kuanza,
hii itatufanya tuwe na wakati mgumu wa kutetea ubingwa wetu kwani tutakuwa
tumechoka,” alisema Cannavaro.
Kuhusu
Yanga kutofanya vizuri kwenye Kombe la Shirikisho, Cannavaro alisema:
“Kinachotuangusha ni kushindwa kuutumia vizuri uwanja wa nyumbani, wenzetu
wakicheza kwao wanapata matokeo mazuri lakini kwetu inakuwa tofauti.
“Hili
ni somo kwetu na kwa kuwa msimu ujao tutashiriki tena, basi tutafuta makosa
yetu, benchi la ufundi nadhani limeona linatakiwa kusajili wachezaji wa aina
gani hasa katika michuano hii ya kimataifa.”
Yanga
inashika mkia katika kundi lake ikiwa na pointi moja tu huku TP Mazembe ikiwa
kinara na pointi 10 ikifuatiwa na Medeama na MO Bejaia ambazo kila moja ina
pointi tano.
Post a Comment