KOCHA Mkuu wa Yanga Mholanzi, Hans Pluijm amemtabiria makubwa beki wake pembeni, Juma Abdul kwa kutamka kuwa kama akiendelea kucheza kwa kiwango hicho, basi atafikia mafanikio ya mshambuliaji wa Genk ya Uturuki, Mbwana Samatta.
Kauli hiyo, aliitoa mara baada ya beki huyo kutangazwa kuwa mchezaji Bora wa Ligi Kuu Bara msimu wa 2015/2016, kwenye Usiku wa Tuzo za ligi kuu zilizofanyika wikiendi iliyopita kwenye Hotel ya Double Tree, Masaki jijini Dar es Salaam.
Abdul, pia alifanikiwa kutwaa tuzo ya Uchezaji Bora wa mwezi Aprili zilizokuwa zinatolewa na Bodi ya ya Ligi Kuu Bara,kabla ya kuichukua ile ya Uchezaji Bora wa Kombe la FA, mwaka huu.
Akizungumza Pluijm alisema Abdul ana kila sababu za kufikia malengo hayo ya kucheza soka la kulipwa kutokana na bidii na kujituma kwake ndani ya uwanja.

“Ninaamini kama Abdul ataendelea na kiwango hicho alichokionyesha misimu hii miwili, ninaamini atamfuata Samatta Ulaya.
“Hilo linawezekana kabisa, kikubwa ni malengo na kujitambua vitu ambavyo wachezaji wengi wa hapa nchini hawana zaidi ya Samatta ambaye aliweka nia akafanikiwa.
“Basi ndiyo itakavyokuwa kwa Abdul, kama akitaka kuweka nia ya kucheza soka la kulipwa, basi anaweza kwa sababu ana kila sababu ya kufanikiwa, ana uwezo wa kupiga krosi, pasi na kona nzuri kwa washambuliaji na kupata mabao,” alisema Pluijm.

Post a Comment

 
Top