OLABA |
TIMU ya soka ya Ruvu Shooting ya mkoani hapa imeachana na
kocha wake Tom Olaba raia wa Kenya licha ya kukirudisha Ligi Kuu Bara kikosi
hicho.
Badala yake, mikoba ya Olaba sasa amekabidhiwa kocha mzawa
Selemani Mtingwe aliyemaliza mafunzo ya ukocha ya leseni daraja B hivi
karibuni.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ofisa Habari wa Ruvu
Shooting, Masau Bwire, Olaba na timu hiyo wameamua kuchana na sasa watakuwa na
Mtingwe aliyekuwa kocha msaidizi.
“Ruvu Shooting tunaheshimu sana mchango wa Olaba katika timu
yetu na tunamheshimu sana Olaba, tutaendelea kumheshimu na kuamini kuwa ni
miongoni mwa makocha bora katika ukanda huu wa nchi za maziwa makuu na Afrika.
“Uongozi wa Ruvu Shooting chini ya Mwenyekiti wake Kanali
Charles Mbuge tunamtakia kila la kheri Olaba, kocha makini, mahili, mcheshi,
mwenye weledi na akili nyingi katika kufundisha soka.
“Ruvu Shooting tunamkumbuka, tutaendelea kumkumbuka kwa mema
na mafanikio makubwa ndani ya timu yetu chini ya uongozi wake,” ilisema sehemu
ya taarifa hiyo ya Bwire.
Olaba alijiunga na Ruvu Shooting msimu wa mwaka 2013/14
mzunguko wa pili baada ya aliyekuwa Kocha Mkuu Boniphace Mkwasa kuvunja mkataba
na kujiunga na Yanga. Msimu wa 2014/15 Ruvu Shooting ilishuka daraja chini ya
Olaba lakini amefanikiwa kuirudisha ligi kuu.
Post a Comment