SIMBA wameingia anga za Ulaya ambao kwa sasa wanatarajia kuuza hisa kwa wanachama ili kubadilisha mfumo wa uendeshaji wa klabu hiyo kongwe hapa nchini.

Klabu kama Arsenal inayoshiriki Ligi Kuu ya England, imekuwa ikijiendesha kwa  mfumo wa kununua hisa ambapo, Stan Kroenke, anaongoza kwa hisa nyingi na mwenye sauti kubwa ndani ya klabu hiyo.

Wanachama wa klabu hiyo, wanatarajiwa kuridhia mfumo mpya wa uendeshaji wa klabu yao katika mkutano mkuu unaotarajia kufanyika Jumapili jijini Dar es Salaam.

Baadhi ya wanachama wa klabu hiyo, wameonyesha nia ya kununua hisa akiwamo bilionia, Mohammed Dewji ‘Mo’, ambaye yuko tayari kununua asilimia 51 kwa thamani ya shilingi bilioni 20.

Rais wa Simba, Evans Aveva na Kamati yake ya utendaji ya klabu hiyo, iliteua kamati ya watu wanne ili kuangalia na kujadili vyanzo vya mapato vya kuweza kusaidia timu yao, ambayo imeleta mapendekezo ya kubadilishwa kwa mfumo wa uendeshaji ili kuifanya Simba ijiendeshe bila kutegemea fedha za mtu kutoka mfukoni.

Katibu wa Kamati hiyo, Mulamu Ng’hambi, alisema walipewa jukumu la kuandaa ripoti ya jinsi hisa itakavyokuwa ikiuzwa kwa wanachama ili waweze kujadili kwenye mkutano wao.

Ng’hambi alisema wametumia miezi miwili kuweka utaratibu wa kuuza hisa za klabu hiyo baada ya kugundua njia pekee ya kukwamua klabu hiyo kiuchumi ni kubadili mfumo wa uendeshaji.

Alisema kamati hiyo iliyokuwa chini ya mwenyekiti wake, Azizi Kefeli ambaye ni mhasibu mkuu wa Serikali ikiwa na wajumbe wawili, Selemani Omari na Ali Sulu, tayari imeandaa ripoti  itakayopelekwa kwa wanachama ili kuridhia mabadiliko hayo.

Ng’hambi alisema kamati yao iliangalia mfumo wa uendeshaji wa klabu hiyo  hasa baada ya kushindwa kufikia malengo yao kwenye Ligi ya Vodacom na michuano mingine na kugundua kwamba tatizo kubwa lilikuwa ni fedha lakini pia mfumo wa uendeshaji wa timu unainyima klabu hiyo kukua kiuchumi.

“Watu wengi wanawalaumu viongozi si kwamba wanashindwa ila wanakwama kwa ajili ya fedha, Simba hawawezi kununua wachezaji wenye viwango vya juu kutokana na mapato yake na vyanzo vyake kuwa ni vichache sana tofauti na timu nyingine,” alisema.

Alisema baada ya kufanya utafiti walibaini sasa ni wakati wa kuwaruhusu watu wengi zaidi kuwekeza fedha zao Simba ikimaanisha wanunue hisa.

Alisema mfumo huo wa kununua hisa hautamwondoa mwanachama yeyote katika klabu hiyo kwani kwa sasa utawapa wanachama nafasi ya kuwa wamiliki wa timu kwa kununua hisa.

“Tumeona ni bora tutengeneze mfumo ambao watu wengi zaidi watawekeza fedha zao na wanunue hisa na fedha hizo zitaweza kutumika kwa manufaa mbalimbali ambapo mtu ambaye atakuwa na hisa nyingi zaidi ndiye atakuwa na sauti zaidi kuliko hizi sasa kila mmoja anaweza kusema na kuamua jambo ambalo linaiyumbisha timu hii,” alisema.

Alisema mtu ambaye atanunua hisa atapewa cheti maalumu cha kumtambua kama mmoja wa wamiliki wa Simba hivyo kila mwanachama anaweza kununua hisa kulingana na uwezo wake.

Ng’hambi alitoa mfano wa klabu ya Arsenal inayojiendesha kwa  mfumo huo wa kununua hisa, ambapo wanahisa wengine ni Alisher Usmonov na Forhad Moshiri ambao wote wana sauti kwenye klabu hiyo.

Alisema kikubwa wanachofanya kwa sasa ni kusambaza elimu kwa wanachama wao ili kuelewa lengo la mfumo huo na kuondoa zile taarifa za watu kupotosha mpango huo.

Ng’hambi alisema kamati hiyo ilifanya mazungumzo na mfanyabiashara maarufu, Mo na amewaambia hana shida ya kuwa mwenyekiti bali ni mwekezaji tu.

“Sisi tulimfuata Mo na kuzungumza naye,  alisema yeye hana shida na cheo chochote Simba na anataka kuwa mwekezaji hivyo tunadhani mfumo huu ndio utakuwa suluhisho kwa klabu hii,” alisema.

Alisema wanatarajia kuwasilisha taarifa yao kwa Kamati ya Utendaji Simba na kupendekeza hoja kwenye Mkutano Mkuu utakaofanyika Julai 31, mwaka huu.

N’ghambi alisema mbali na Mo kujitokeza kununua hisa kuna matajiri wengine kama Azim Dewji na wengineo.

“Yaani kuna watu wengi sana ambao wameonyesha nia ya kuridhika na mfumo huu siwezi kuwataja kwa sasa ila ni wengi, mfumo huu utaweza kuisaidia Simba,” alisema.
CHANZO: DIMBA

Post a Comment

 
Top