KIROHO safi Simba
imekubali yaishe kwa straika Laudit
Mavugo kwamba haitampata tena, lakini imeweka mkakati wa kuhakikisha
inamfuata Ufaransa ili arudishe fedha zao Sh milioni 36.
Mwaka jana, Simba ilimpa Mavugo kiasi hicho
cha fedha lakini kumbe ilikuwa sawa na bure kwani alikuwa na mkataba na Vital’O
ambayo ilidai fedha ndefu ili imwachie straika huyo.
Simba haikuwa na fedha hiyo ikaamua kutulia
ikiamini straika huyo atajiunga nao pindi akimaliza mkataba na Vital’O, ajabu
Mavugo alipomaliza mkataba akauchuna.
Kuona hivyo Simba ikamtuma kiongozi wake mmoja
kumfuata Mavugo nchini Burundi, lakini bosi huyo akaishia kuonana na katibu wa
Vital’O bila kumuona rais wa timu hiyo, Bikolimana Benjamini anayesimamia haki
za straika huyo.
Bosi huyo wa Simba akaamua kugeuza zake na
kurudi Dar es Salaam huku nyuma Mavugo akipelekwa Ufaransa.
Habari kutoka Simba zinasema, klabu hiyo sasa
imetegeshea Mavugo akisajiliwa tu Ufaransa watamfuatilia na kudai fedha yao Sh
milioni 36 walizompa.
“Mavugo hawezi kuja tena, kiongozi wetu mmoja
aliyetumwa Burundi ameshindwa kuzungumza na rais wa Vital’O ambaye ndiye aliyegomea
Mavugo kuja Simba. Kutokana na hali hiyo sasa tunasubiri fedha yetu.
“Mavugo akipata timu Ufaransa tutamfuata na
kudai fedha yetu, wala hatugombani naye,” alisema bosi huyo wa Simba.
Post a Comment