KIKOSI cha Yanga kimerejea jana nchini
kwa mafungu kikitokea nchini Ghana kilipokuwa kimeenda kwa ajili ya mechi yake
ya marudiano ya kimataifa ya kuwania Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya
Medeama ya nchini humo.
Timu hiyo imerejea ikiwa na machungu
kibao iliyoyapata baada ya kutandikwa mabao 3-1, Jumanne ya wiki hii hali
iliyoifanya izidi kujiweka katika mazingira magumu ya kutinga hatua ya nusu
fainali ya michuano hayo.
Hata hivyo mabeki wa kati wa timu
hiyo, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ na Kelvin Yondani, wamejikuta katika wakati
mgumu kutoka kwa baadhi ya mashabiki wa timu hiyo mara baada ya kutua katika
Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam usiku wa
kuamkia jana.
Baadhi ya mashabiki walisikika wakiwatuhumu
Cannavaro na Yondani kuwa waliifungisha timu hiyo huku wakidai kuwa endapo
mechi hiyo angecheza, Mtogo, Vincent Bossou pengine hayo yote yasingetokea.
Mashabiki hao baada ya kuona kuwa
maneno yao hayo hayatafika popote waliamua kumsubiri kocha mkuu wa timu hiyo,
Hans van Der Pluijm ambaye alikuja katika ndege tofauti na wachezaji hao na
kumtaka achukue hatua kali dhidi ya wachezaji hao.
Mara baada ya mashabiki hao kulalamika
kwa Pluijim, kocha huyo alisema: “Nimewasikia na nitayafanyia kazi maoni yenu
hayo kwani hata mimi hilo nililiona.”
Yanga inaburuza mkia katika kundi lake
ambalo ipo na timu za TP Mazembe ya DR Congo, Medeama ya Ghana na MO Bejaia ya
Algeria.
Post a Comment