KATIKA kuhakikisha Simba inarudisha heshima yake ambayo imepotea kwa muda mrefu, imeamua kuunda upya kikosi chake kitakachokuwa na ushindani mkubwa na kukabiliana na kasi ya wapinzani wao wa jadi, Yanga.
Hata hivyo, uongozi huo wa Simba unatarajia kutumia zaidi ya shilingi milioni 200 ili kuhakikisha mpango huo unatimia kwa kusajili wachezaji wa kiwango cha juu na tayari umeshaanza mikakati hiyo.
Hadi hivi sasa, Simba tayari imeshasajili wachezaji sita wazawa kwa kuzingatia upungufu iliouona katika kikosi cha timu hiyo cha msimu uliopita walipomaliza katika nafasi ya tatu.
Wachezaji hao ni Jamal Mnyate na Emmanuel Semwanza (Mwadui), Mohammed Ibrahim,  Mzamiru Yassin (Mtibwa Sugar), Hamad Juma (Coastal Union) na Shiza Kichuya (Mtibwa Sugar).
Mnyate ambaye ni kiungo mshambuliaji anayecheza winga wa kushoto namba 11, amesajiliwa ili kuiongezea nguvu safu ya ushambuliaji timu hiyo ambayo ilikosa ufanisi mkubwa tangu alipoondoka Ramadhan Singano ‘Messi’ ambaye yupo Azam FC.

Nafasi hiyo kwenye msimu uliopita ilikuwa haina mchezaji maalum wa kucheza, walikuwa wakibadilishana wakati mwingine alikuwa akicheza Hijja Ugando na muda mwingine Mwinyi Kazimoto, hivyo msimu ujao Mnyate anatarajiwa kukutana na ushindani kutoka kwa nyota hao.
Kwa upande wa Semwanza ambaye ni beki wa kati anayemudu kucheza namba tano, yeye ameletwa kwa ajili ya kuchukua nafasi ya Hassan Isihaka ambaye alishindwa kumudu kucheza nafasi hiyo, kabla ya kutemwa na Novatus Lufunga kupewa nafasi ya kucheza katika kikosi msimu uliopita wa ligi kuu, hivyo Semwanza anatarajiwa kupambana ili kumtoa mwenyeji huyo katika kikosi cha kwanza, hiyo ni baada ya Mganda, Juuko Murshid kujihakikishia nafasi ya kudumu.
Ibrahim anayemudu kucheza nafasi ya kiungo namba nane, yeye anatarajiwa kukutana na ushindani mkubwa wa namba kutokana na rundo kubwa la viungo lililojaa Simba ambao ni Said Ndemla, Mwinyi Kazimoto na Peter Mwalyanzi, hivyo anatakiwa kupambana ili apate nafasi ya kucheza kwenye kikosi cha kwanza. 
Kwa Mzamiru yeye ana bahati kwa kuwa ni kiraka, anamudu kucheza nafasi za kiungo namba nane, pia kumi aliyokuwa anaicheza msimu uliopita akiwa na Mtibwa Sugar, yeye anatarajiwa kupambana msimu ujao wa ligi kuu ili apate nafasi ya kucheza mbele ya Danny Lyanga ambaye amemkuta kwenye timu hiyo.

Hamad yeye amesajiliwa kwa ajili ya msimu ujao wa ligi kuu ili achukue nafasi ya Hassan Kessy aliyetimkia Yanga na Mrundi, Emiry Nimubona aliyetimka kwenye timu hiyo mara tu baada ya mkataba wake kumalizika.
Kwa upande wake winga, Kichuya yeye aliletwa klabuni kuziba pengo la Mganda, Brian Majwega ambaye Wanasimba wengi walimuamini na kuona kuwa anaweza kuwasaidia lakini mambo yakawa ndivyo sivyo na akajikuta akifungashiwa virago.
Ukiachana na hayo, pia ujio wa wachezaji hao utasababisha wengine waliokuwa wakitumikia timu hiyo msimu uliopita kupoteza nafasi zao kwenye kikosi cha kwanza kama wasipokuwa makini.
Kutokana na usajili huo wa Simba ambao imeufanya mpaka sasa, kikosi chake kinaweza kuwa hivi. Vincent Angban, Hamad Juma, Abdallah Hussein ‘Zimbwe Jr’, Novatus Lufunga, Juuko Murshid, Jonas Mkude, Jamal Mnyate, Mzamiru Yassin, Daniel Lyanga, Ibrahim Ajibu na Shiza Kichuya.
Hali hiyo itawafanya makipa, Peter Manyika na Denis Richard, mabeki, Emmanuel Semwanza, Abdi Banda na Said Issa, viungo, Said Ndemla, Peter Mwalyanzi, Mwinyi Kazimoto, Mohamed Ibrahim na Awadhi Juma, washambuliaji, Mussa Hassan ‘Mgosi’ na Hijja Ugando kuwa wachezaji wa akiba.
Hata hivyo kikosi hicho kinaweza kubadilika endapo tu uongozi huo utawasajili wachezaji wa kimataifa wanaoendelea kufanya majaribio na timu hiyo mkoani Morogoro.

Post a Comment

 
Top