AKIWA na wiki tatu tu ndani ya
kikosi cha Simba, Kocha Joseph Omog amesema kwa jinsi alivyoiandaa timu yake,
tayari imeonyesha mwanga wa kutwaa ubingwa au kupata nafasi ya kucheza michuano
ya kimataifa.
Kauli hiyo ya Omog, raia wa Cameroon, imekuja ikiwa ni
wiki tatu pia tangu asaini mkataba wa miaka miwili kuifundisha Simba.
Omog aliiambia SPOTIRIPOTABLOG, jana kwamba: “Kimoja lazima tukipate, kama siyo ubingwa basi tucheze
michuano ya kimataifa.”
Bingwa wa Ligi Kuu Bara ndiye anayepata nafasi ya
kuiwakilisha Tanzania katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na mshindi wa
Kombe la FA pia hupata nafasi ya kushiriki Kombe la Shirikisho Afrika.
Jana Ijumaa Simba ilifanya mazoezi mepesi kwenye Uwanja
wa Chuo cha Biblia cha Highlands mjini hapa kabla ya jioni kucheza mechi ya
kirafiki dhidi ya Moro Kids.
Omog alisema: “Najua kwa miaka minne sasa Simba
imeshindwa kupata mafanikio, kitu ambacho Wanasimba wengi wanakitamani kitokee
msimu ujao.
“Nimepewa dhamana hiyo na nawaahidi kwa maandalizi haya
tunayoyafanya, tusipokuwa mabingwa (wa ligi kuu), basi lazima tushiriki
michuano ya kimataifa, hayo ndiyo malengo yetu kwa msimu ujao.
“Vijana wapo kwenye hali nzuri na wanaendelea kujifua
kwa ajili ya msimu ujao, wenzetu walikuwa bora msimu uliopita, lakini msimu
ujao utakuwa wetu.”
Post a Comment