HUU sasa ni uchokozi wa wazi kabisa, kwani Yanga imefanya umafia kwa kuuchungulia mkataba wa mshambuliaji wa Simba, Ibrahim Ajib kisha ikapiga dole.

Ajib, aliyetwaa Tuzo ya Bao Bora la Msimu wa Ligi Kuu Bara 2015/2016 aliyekuwa anachuana na mshambuliaji wa Yanga Mrundi, Amissi Tambwe, kuna wakati alihusishwa na kujiunga na Yanga lakini mambo yakashindikana.

Wakati huo mambo yalisukwa hivi, Ajib aliwekewa mpango wa kwenda kufanya majaribio Afrika Kusini kumbe wakati huohuo mipango ya kusajiliwa na Yanga ikawa inasukwa kimtindo.


Yanga ikaamua kuishia njiani baada ya kubaini kuwa, Ajib bado ana mkataba wa mwaka mmoja, hivyo wakanywea na kurudi nyuma, ila timu hiyo ikajiongeza katika hatua zake za kumfuatilia straika huyo.

Mmoja wa mabosi wa Kamati ya Mashindano ya Yanga na wenzake walitinga kwenye Ofisi za Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kinyemela na kupekuwa ‘document’ za mkataba wa mchezaji huyo na kujua tarehe, mwezi na mwaka ambao unamalizika.

Bosi huyo alisema, uongozi ulifikia hatua hiyo ya kuupekuwa mkataba huo, baada ya mshambuliaji huyo kutoweka wazi kilichoandikwa ndani yake, hivyo kuwapa shaka katika kumsajili.

“Ajib alikuwepo kwenye mipango yetu ya kumsajili, lakini mipango hiyo ilipotea baada ya kuingia utata wa mkataba wake ambapo Simba walidai amebakisha mwaka mmoja huku mwenyewe akidai umemalizika.


“Hivyo, tukaona tuepushe utata kama uliopo hivi sasa kati yetu na Simba (kuhusu Hassan Kessy) ambayo hadi hivi sasa imegomea kutupa barua ya kumuidhinisha kuichezea Yanga, tukajiongeza kidogo.

“Tumeona ni vyema tukafuata kanuni za usajili ikiwemo kujua tarehe na mwaka rasmi ambao mkataba wake (Ajib) unamalizika, hivyo tunashukuru tumeshajua tayari na muda tunamalizana naye,” alisema bosi huyo.

Alipotafutwa Ajib kuzungumzia hali hiyo alisema: “Nisingependa kuzungumzia kuhusiana na Yanga, mimi niliomba kwa viongozi kuruhusiwa kwenda kucheza soka la kulipwa Afrika Kusini pekee na siyo kitu kingine.”

Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zakari Hans Pope aliwahi kusema kuwa, Ajib hataenda popote na badala yake atabaki kuichezea timu hiyo hadi mkataba wake utakapomalizika.

Post a Comment

 
Top