MUDA wowote kuanzia leo, Kocha wa Yanga, Hans van Der Pluijm atakabidhi kwa uongozi ripoti yake ya mchezo uliopita wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Medeama ambao walifungwa mabao 3-1.
Yanga ilifungwa na Medeama, Jumanne wiki hii nchini Ghana na kuzima matumaini ya kucheza nusu fainali katika michuano hiyo kutoka Kundi A kwani ina pointi moja tu huku kinara TP Mazembe ikiwa na pointi 10.

Inahitajika miujiza ili Yanga itinge nusu fainali kwani Medeama ipo nafasi ya pili ikiwa na pointi tano sawa na MO Bejaia iliyopo nafasi ya tatu. Timu zote zimebakisha mechi mbili
Ripoti hiyo ya Pluijm inatarajiwa kuwa na mambo mengi kwani juzi Alhamisi baada ya kuwasili nchini kutoka Ghana, aliwatupia lawama mabeki wake kwa kusema ndiyo chanzo cha kufungwa.
Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Yanga, Hussein Nyika alisema muda wowote kuanzia leo, Pluijm atakabidhi ripoti hiyo kwa uongozi.

“Kuna mambo mengi tuliyaona katika mechi hiyo lakini kwa sasa hatuwezi kufanya lolote mpaka tutakapopata ripoti ya kocha ambayo atatupa muda wowote kuanzia kesho (leo),” alisema Nyika.
Alipoulizwa Pluijm kuhusiana na ripoti yake hiyo, alisema: “Tayari nimeshaiandaa na muda wowote nitaikabidhi kwa uongozi.”
Yanga itacheza na MO Bejaia ya Algeria, Agosti 13, mwaka huu jijini Dar es Salaam halafu itaenda Lubumbashi, DR Congo kucheza na TP Mazembe kati ya Agosti 23 na 24, mwaka huu.



Post a Comment

 
Top