JANA, Jumanne timu ya Yanga
ilishuka uwanjani kupambana na Medeama katika mchezo wa marudiano wa Kombe la
Shirikisho Afrika uliofanyika kwenye Uwanja wa Essipong Sports mjini Sekondi
nchini Ghana na wawakilishi hao kupigwa mabao 3-1.
Hata hivyo, wachezaji baadhi
wa Yanga wameipigia saluti Medeama kwa fitna kabambe ilizowafanyia wakati
walipotua Ghana kwa ajili ya mchezo huo ambazo zilifanya waingiwe na hofu kubwa
ya kutekwa walipokuwa njiani wakitokea Accra kwenda Sekondi.
Wakizungumza kwa nyakati
tofauti wachezaji hao ambao ni, kipa Deogratius Munishi na mshambuliaji wa timu
hiyo, Mrundi, Amissi Tambwe walidai kuwa baada ya kutua katika Uwanja wa Ndege wa
Kimataifa wa Accra, ilikuwa ni usiku na walijua kutoka hapo kwenda Sekondi
wangepewa ulinzi kutokana na umbali ambao wangesafiri kwa basi.
“Hata hivyo, hali haikuwa
kama tulivyotarajia, tulisafiri usiku huo kwa basi tena kwa zaidi ya saa tano
bila ya kuwa na ulinzi wa aina yoyote, hakika kila mtu ndani ya basi alikuwa
akimwomba Mungu kila tulipokuwa tukifikiria hali ya usalama katika mataifa haya
ya Magharibi.
“Akili zetu zilitawaliwa na
hofu kubwa kwani tulikuwa tukipita sehemu nyingine zilikuwa ni mapori, hata
hivyo hofu hiyo ilishuka baada ya kufika Sekondi na ndipo tulipoanza kutaniana
huku baadhi yetu tukiona hali hiyo kama bonge la fitina ambalo wapinzani wetu
walitufanyia kwa sababu walituvuruga kwa kiwango kikubwa,” alisema Dida.
Kwa upande wa Tambwe alisema:
“Ilikuwa ni balaa tulifika tumechoka sana na hakuna mtu aliyekuwa akiamini kama
tutafika salama Sekondi kutoka Accra ila tunamshukuru Mungu kwa hilo ila jamaa
nimewakubali kwa fitna hiyo ya soka.”
Post a Comment