WAKATI benchi la
ufundi la timu ya Simba likiendelea kuwafanyia tathimini baadhi ya wachezaji
wake wa kimataifa wanaofanya majaribio ya kutafuta nasafi ya kusajiliwa kwa
ajili ya msimu ujao, uongozi wa klabu hiyo unatarajia kushusha straika mpya
kutoka nchini Ghana.
Kwa jinsi mipango ilivyo, straika huyo
anatarajiwa kutua nchi leo au kesho na kwenda moja kwa moja mkoani Morogoro
kuungana na kikosi cha timu hiyo kilichojichimbia huko kwa ajili ya maandalizi
yake ya msimu ujao wa Ligi Kuu Bara unaotarajiwa kuanza kutimua vumbi Agosti 20,
mwaka huu.
Atakapofika huko, straika huyo ambaye jina
lake halikuweza kupatikana mpaka tunaenda mitamboni, atafanyiwa majaribio na
Kocha Mkuu wa Simba, Mcameroon, Joseph Omog ambaye anaendelea na harakati zake
za kukisuka upya kikosi hicho.
Habari za kuaminika kutoka ndani ya Simba
zimedai kuwa ujio wa straika huyo klabuni hapo umetokana na uongozi wa klabu
hiyo kufanyiwa mipango na baadhi ya maofisa wa timu ya soka ya Medeama ambao
waliwaomba wawatafutie mshambuliaji wakati
walipokuwa hapa nchini na kikosi chao kwa ajili ya mechi ya kimataifa ya
Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Yanga.
“Ni kweli kabisa kesho au keshokutwa Jumanne
tunaweza kumpokea straika mpya kutoka Ghana ambaye anakuja kufanya majaribio na
endapo ataonyesha uwezo wa juu utakaomridhisha kocha basi tutamsajili.
“Straika huyo tumefanyiwa mipango na baadhi ya
viongozi wa Medeama ya Ghana ambao tuliwaomba watutafutie wakati walipokuwa
hapa nchini na kikosi chao kwa ajili ya kucheza na Yanga katika mchezo wa Kombe
la Shirikisho Afrika,” kilisema chanzo hicho cha habari.
Alipotafutwa Katibu Mkuu wa Simba, Patrick
Kahemele ili azungumzie suala hilo hakupatikana, lakini alipotafutwa makamu wa
rais wa klabu hiyo, Geofrey Nyange
‘Kaburu’ alipatika na alipoulizwa alionyesha mshangao kisha akauliza: “Nani
kakwambia jambo hilo, hakuna kitu kama hicho, siku ile ya mechi ya tulikwenda
kuwapongeza tu Medeama na hakuna kitu kingine tulichozungumza nao lakini kama
kuna lolote itajulikana.”
Post a Comment