MASHABIKI wa Arsenal sasa hivi wapo
kwenye maombi ya kumshawishi kocha wa timu hiyo, Arsene Wenger asaini beki
mwingine wa kati baada ya Per Mertesacker kuumia.
Hii siyo kwa kuwa kocha huyo Mfaransa
anataka yeye kusajili hapana, bali ni kutokana na kutokuwa na mchezaji mbadala
ambaye anaweza kucheza nafasi ya Mertesacker atakayekuwa nje ya uwanja kwa muda
mrefu.
Mertesacker alikuwa apewe unahodha
kutoka kwa Mikel Arteta ambaye amestaafu na kuamua kutimkia Man City akiwa kama
kocha msaidizi wa Pep Guardiola.
Mertesacker anatarajiwa kuwa nje ya
uwanja kwa muda wa miezi mitano akiuguza goti aliloumia kwenye mchezo wa
kirafiki dhidi ya RC Lens Ijumaa iliyopita.
Beki huyo amekuwa na kiwango cha
kupanda na kushuka huku akionekana kutengeneza pacha nzuri na Laurent
Koscielny. Lakini sasa kutokana na kuumia kwa beki huyo Mjerumani, hawa ni
baadhi ya mabeki ambao wanaweza kucheza nafasi yake kikamilifu endapo
watasajiliwa;
Shkodran
Mustafi
Beki huyu Mjerumani anatajwa kuwa
mmoja kati ya walinzi wanaoweza kuziba pengo la Mertesacker kwa ukamilifu. Umri
wake wa miaka 24 unamfanya kuwa atadumu kwa muda mrefu zaidi na Arsenal kwani
ukiangalia Mertesacker sasa hivi ana umri wa miaka 31.
Mustafi sasa hivi anachezea Valencia, anasifika
kwa kujua kujipanga, kulinda kwa ufasaha na kuuchezea mpira. Hata hivyo amekuwa
akihusishwa pia kutua Arsenal.
Benedikt
Howedes
Mashabiki wa Arsenal wanaonekana pia
kuvutiwa na beki Howedes na wanamtaka wenger amsajili ikiwa atamkosa Mustafi.
Mlinzi huyo ambaye ni mshindi wa Kombe
la Dunia akiwa na Ujerumani mwaka 2014 ni nahodha wa Klabu ya Schalke 04,
inayoshiriki Ligi Kuu ya Ujerumani ‘Bundesliga’. Beki huyu mwenye umri wa miaka
28 anatajwa kuwa ni mlinzi imara na ataweza kuuziba vyema ukuta wa Arsenal
sambamba na Koscielny, Hector Bellerin na Nacho Monreal.
Howedes mpaka sasa amedumu kwenye
kikosi hicho kwa miaka 15 na Februari alisaini dili jipya la kuendelea kuwepo Schalke
04 lakini Arsenal wanaweza kumshawishi ajiunge nao.
Kalidou
Koulibaly
Huyu pia aliwahi kutajwa kipindi cha
nyuma kutakiwa na Arsenal, anaitwa Koulibaly. Jamaa ni mrefu na yupo fasta
uwanjani.
Nyota huyu sasa anachezea Napoli ya
Italia na amekuwa kwenye kiwango kizuri sana tangu alipojiunga nayo akitokea
Racing Genk.
Kostas
Manolas
Manolas anatajwa kuwa mmoja kati ya
mabeki walio kwenye kiwango cha juu sasa hivi, hivyo anaweza kuwa wa gharama.
Beki huyu raia wa Ugiriki amekuwa akizivutia klabu nyingi Ulaya lakini mara
nyingi amekuwa akisema anabaki Roma ya Italia.
Chelsea ni moja kati ya klabu
iliyotajwa kumtaka lakini akaitolea nje, huyu anaweza kuwa jibu tosha katika
kuziba pengo la Mertesacker pale Arsenal lakini Wenger anatakiwa kutoa ‘mpunga’
wa maana kwani thamani yake imekuwa ikiripotiwa kupanda mara kwa mara. Anaweza
kuwagharimu Arsenal pauni milioni 30 (Sh bilioni 84.3).
Post a Comment