KIKOSI cha Yanga
kiliondoka nchini juzi Jumamosi alfajiri kuelekea Ghana kikiwa na wachezaji 21
na viongozi tisa wakiongozwa na Mwenyekiti wa Chama cha Wachezaji wa Soka
Tanzania (Sputanza), Musa Kisoki, kwa Ndege ya Shirika la Kenya Airways huku
wakionekana ni wenye matumaini kibao.
Lakini inaonekana kama wenyeji wao Medeama SC
ya Ghana wameweka fitna mbele baada ya kuipeleka mechi hiyo mbali kwenye uwanja
mdogo wa Sekondi-Takoradi unaochukua watu 20,000, kwani Yanga walilazimika
kusafiri hadi usiku na kufika wakiwa wamechoka sana.
Yanga ilifika jijini Accra majira ya saa 12
jioni kwa saa za Ghana, Tanzania ikiwa ni saa tatu usiku na kulazimika kusafiri
usiku huohuo hadi kufika kwenye mjini wa Tarkwa walikofika saa tano usiku kwa
saa za huko ikiwa ni saa nane usiku kwa Tanzania. Walitumia basi lililoandaliwa
na wenyeji wao ambalo lilitakiwa kusafiri usiku huohuo kuwapeleka wanapotaka
kwenda.
Hofu nyingine ya hujuma ni kutokana na uwanja
kuwa mbali na Accra hali ambayo inaonyesha ni kama ilivyotokea kwenye mchezo wa
kufuzu hatua ya makundi dhidi ya Sagrada Esperanca ambapo Yanga walifanyiwa
hujuma nyingi wakiwa kwenye uwanja mdogo wa timu hiyo.
Hali hii inaonyesha kuwa Uwanja wa Sekondi upo
karibu na nyumbani kwa Medeama, kuna wasiwasi kwamba huenda mambo ya hujuma
yanaweza kuhusika.
Yanga itacheza na Medeama katika mchezo wa
Kombe la Shirikisho Afrika kesho Jumanne majira ya saa tisa kwa saa za Ghana
huku Tanzania ikiwa ni saa 12:00 jioni.
Lakini kama ilivyokuwa katika mchezo wa kwanza
kwenye Uwanja wa Taifa, Dar baina ya timu hizo, waamuzi wa mechi hiyo walitoka
kwenye nchi ya Kiarabu ya Misri na huku Ghana waamuzi wanatoka kwenye ukanda
huohuo ambapo sasa wanatokea Morocco.
Hata hivyo, Yanga ambao wanaonekana kupambana
na fitina za Waghana hao jana saa 12 jioni kwa saa za Tanzania walifanya
mazoezi yao na kuonekana wachezaji wote wakiwa na morali ya hali ya juu.
Washambuliaji wawili wa timu hiyo, Mrundi
Amissi Tambwe na Simon Msuva wamedai kuwa kesho watapambana kufa na kupona ili
kuhakikisha Yanga inaibuka na ushindi katika mechi hiyo. Yanga inahitaji
ushindi tu ili kufufua matumaini ya kutinga nusu fainali.
Wakizungumza na Championi Jumatatu wakiwa nchini Ghana, wachezaji hao wamedai kuwa
mechi hiyo ndiyo fainali yao kwani wakipoteza basi huo ndiyo utakuwa mwisho wao
wa kusonga mbele katika michuano hiyo.
“Tunamshukuru Mungu kwa kila kitu kwani tupo
vizuri mpaka sasa lakini jambo kubwa ambalo linatuumiza vichwa ni mechi yetu ya
Jumanne dhidi ya Medeama.
“Tangu tunatoka Dar es Salaam akili yangu yote
inafikiria mechi hiyo, hakika sina cha kusema zaidi ya kuhakikisha siku hiyo
tunaibuka na ushindi hata kama ni kufia uwanjani ni bora iwe hivyo,” alisema
Msuva.
Kwa upande wake, Tambwe alisema: “Tuna kazi
kubwa ya kufanya ili kufufua matumaini yetu ya kusonga mbele katika michuano
hii, vinginevyo huo ndiyo utakuwa mwisho wetu.
“Binafsi namuomba Mungu anijalie uzima ili
tuweze kuibuka na ushindi katika mchezo huo.”
Post a Comment