WAKATI uongozi wa Simba ukidai kuwa hadi hivi sasa haujui hatima ya ujio wa mshambuliaji Mrundi, Laudit Mavugo, meneja wa mchezaji huyo na mmiliki wa Klabu ya Vital’O ya Burundi, Benjamin Bikolimana amefunguka kuwa Mavugo ametimkia nchini Ufaransa katika mapumziko.
Mshambuliaji huyo ambaye alitarajiwa kutua leo Jumatatu kwa ajili ya kuanza maandalizi ya msimu mpya wa Ligi Kuu Bara chini ya Kocha wa Simba, Mcameroon, Joseph Omog, dalili zinaonyesha hatatua, kwani imeshangaza badala ya kuja kazini amekwenda kula bata Ufaransa.

Ikumbukwe kuwa, mwaka jana Simba ilimpa Mavugo Sh milioni 36 kama ada ya usajili lakini timu yake ya Vital’O ikakataa ikisema nayo ilipwe kwani ilikuwa na mkataba na straika huyo.
Akizungumza moja kwa moja kutoka nchini Burundi, Bikolimana ambaye pia ni meneja wa mchezaji huyo, alisema kuwa kwa sasa hajui chochote kuhusu Simba zaidi ya Mavugo kwenda zake nchini Ufaransa katika mapumziko akiwa na familia yake.
“Nina muda sijazungumza na Mavugo na wala hatujazungumza kuhusiana na suala la Simba kwa sababu nakumbuka hiyo ilikuwa mwaka jana na ilishindikana kutokana na kushindwa kufikia makubaliano ya kuwauzia mchezaji huyo.

“Ninavyojua ni kwamba, hayupo hapa nchini, amekwenda zake katika mapumziko huko Ufaransa na sijui lini atarejea hapa Bujumbura, sasa unanieleza anakuja Tanzania kuichezea Simba mimi hilo siwezi kuliongelea kwani ni vyema akatafutwa mwenyewe awaeleze kuhusu hilo,” alisema Bikolimana. 
Rais wa Simba, Evans Aveva, hivi karibuni alilalamika kuwa wameshampa mchezaji huyo fedha zote zinazotakiwa lakini anashangaa kwa nini haji nchini kutumika.





Post a Comment

 
Top