Rais wa TFF, Jamal Malinzi
KOCHA wa makipa wa Simba, Adam Abdallah ‘Meja’, analazimika kuikacha kambi ya timu hiyo iliyopo mkoani Morogoro baada ya kutakiwa kurudi darasani kwa ajili ya kozi ya ukocha iliyoandaliwa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
Kozi hiyo ya Leseni C, inatarajiwa kuanza mapema mwezi ujao na itadumu kwa siku tano ambapo mafunzo hayo yatafanyika kwenye Uwanja wa Karume zilizopo Ofisi za TFF jijini Dar.
Meja alisema Julai 30, mwaka huu, ataondoka kambini Morogoro na kuja Dar kwa ajili ya kozi hiyo ambayo anaamini itamuongezea ujuzi kwani lengo lake siku moja ni kuifundisha timu ya taifa, Taifa Stars.

“Ni kweli nitaachana na kambi ya huku Morogoro kwa ajili ya kuja kusomea kozi ya ukocha ngazi ya juu, hapo awali kulikuwa na kozi nyingine kama hii ambayo nilihudhuria, lakini hii ya sasa ni kama awamu ya pili.
“Julai 30 nitaondoka huku Morogoro na kuwaacha wenzangu wakiendelea na kambi, kozi yetu itachukua takribani siku tano mpaka kukamilika, kozi kama hizi ni muhimu kwetu na nitakuwa nahudhuria kila zikitokea kwani lengo langu ni kuja kuwa kocha mkubwa hapa nchini ili siku moja niifundishe Taifa Stars,” alisema Meja.

Post a Comment

 
Top