KIKOSI cha
Yanga kilirejea jijini Dar, usiku wa kuamkia jana kikitokea Ghana ambapo
kilipata kichapo cha mabao 3-1 katika mechi ya Kombe la Shirikisho Afrika
ambapo kuna mengi yametokea baada ya matokeo hayo.
Kocha abanwa
Mara baada
ya Kocha wa Yanga, Hans van Der Pluijm kutua katika Uwanja wa Ndege wa
Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Dar, kocha huyo hakutaka kuvunga moja kwa
moja lakini akionyesha kuwa na masikitikio alisema mabeki wake ndiyo waliofanya
makosa na kuruhusu mabao waliyofungwa.
Pluijm
alisema makosa ya mabeki yaliyotokea ni yaleyale ambayo amekuwa akiwaambia kila
mara.
“Kila siku
ni makosa yaleyale, mabeki wa kati na wa pembeni wanakosa mawasiliano, aina ya
mabao tunayofungwa ni yaleyale. Tumefundishana sana mazoezini jinsi ya kukaba
kwamba tufanye nini tunapokuwa na mpira na tunafanya vipi tukikosa mpira lakini
bado mambo ni yaleyale.
“Kwa muda
mrefu tunafanyia kazi suala la kukaba na kila mmoja anaelewa majukumu yake hata
kama ukiwa straika lakini mwishowe ni yaleyale tu.
“Unaona mtu
anashindwa kujipanga kuokoa shambulizi ambalo katika mechi iliyopita alifungwa
bao kupitia dizaini hiyohiyo.
“Kama ni
kufundisha tayari tumefanya kila kitu mazoezini, kilichobaki najua nitafanya
nini. Haya makosa hayahitajiki tena kwa hapa tulipofikia, najua nini cha
kufanya, tutalimaliza hili,” alisema Pluijm, kocha wa zamani wa Medeama na
Berekum Chelsea za Ghana.
Pamoja na
hayo, lakini kocha huyo bora wa Ligi Kuu Bara msimu wa 2015/16, aliweka wazi
kuwa bado hajakata tamaa kwa matokeo hayo na kwamba katika ulimwengu halisi wa
soka wanahitaji kupambana mpaka mwisho katika mechi hizi mbili zilizobaki na
lolote linaweza kutokea.
“Mechi bado
hazijaisha na tunahitaji ushindi wa hali na mali katika mechi zilizobaki,
hatuwezi kukata tamaa, katika soka lolote linatokea. Nikwambie tu kwamba
tunahitaji ushindi wa mabao mengi katika mechi hizi mbili zilizosalia,” alisema
Pluijm.
MKUU WA
MSAFARA AFUNGUKA
Pamoja na
hayo, mkuu wa msafara huo, Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Shirikisho la Soka
Tanzania (TFF), Mussa Kisoki, alitoa maoni yake kuwa kama Yanga inahitaji
kubadilika ni lazima ikubali kuachana na wachezaji wengi wa kikosi cha kwanza
ambao umri wao umekwenda na hawana tena kasi ya ushindani.
“Binafsi
baada ya mechi nimemwambia Pluijm kwamba timu inahitaji mabadiliko, timu ina
watu umri wao umekwenda, hawawezi mikikimikiki, wale Medeama wana vijana wa
miaka 20, 23 na 25, wanacheza soka kwelikweli, walikuwa wanawapeleka puta kina
Yondani.
“Kikosi
kinatakiwa mabadiliko, wapewe nafasi hawa kina Dante (Andrew Vincent) kila
mmoja ameona kazi yao msimu uliopita, wacheze waisaidie timu.
“Nashukuru
Pluijm ameonyesha kunielewa kwa nilichomwambia, maana kwa kuchukua ubingwa
Tanzania haitoshi kuonyesha kuwa una timu bora sana ya kupambana Afrika.
“Kingine
wachezaji hawakufuata maelekezo ya mwalimu. Nilikuwepo mazoezini na
aliwaelekeza kutumia mawinga na jinsi gani namba nane, tisa na 10 wajipange kwa
ajili ya kupokea mipira ya kufunga lakini haikuwa hivyo, walicheza tofauti.
“(Donald) Ngoma
naye siyo straika wa kumuwekea sana matumaini kimataifa kutokana na staili yake
ya uchezaji, mara nyingi anapokea mipira akiwa kaligeukia goli la wapinzani na
hana ‘option’ ya kumkimbia beki akiwa katika hali hiyo, anachokifanya
anarudisha mipira nyuma, Yanga inahitaji mabadiliko,” alisema Kisoki.
UONGOZI NAO
VIPI?
Katika ngazi
ya uongozi wa Yanga kupitia kwa Hussein Nyika ambaye ni mjumbe wa kamati ya
mashindano alizungumza machache:
“Makosa
tumeyaona katika mechi hizi lakini hatuwezi kufanya lolote zaidi ya kusikilizia
ripoti na maagizo ya mwalimu, kiufundi yeye ameonaje na anatakaje kisha sisi
tutafanya kama alivyoagiza, kama ni kusajili wapya au kurekebisha kitu gani,
tutafanya hilo.
“Kimsingi
katika mechi zilizobaki hatuwezi kuwakatisha tamaa wachezaji kuwa hapa ndiyo
mwisho, mashindano ni mashindano, tunahitaji kupigana katika mechi mbili
zilibaki, kisha baada ya hapo tutaangalia kilichopatikana,” alisema Nyika.
Yanga
imebakiza michezo miwili tu, mmoja itakuwa nyumbani dhidi ya MO Bejaia na mwingine
ni ugenini dhidi ya Mazembe.
WACHEZAJI
NAO WANENA
Hata hivyo,
wachezaji waliorejea pamoja na benchi la ufundi la timu hiyo; Dante na Juma
Mahadhi walizungumza na Championi Ijumaa kuhusiana na mchezo huo.
“Matokeo
hayo hatujayafurahia, kikubwa ni kocha kutupatia nafasi ya kucheza na nitakuwa
bora zaidi kwa ajili ya kuifanyia makubwa Yanga, hii ni mechi yangu ya kwanza
ya kimataifa nikiwa na Yanga na nashukuru nimecheza vizuri, hivyo nafikiri
baada ya mechi kadhaa nitakuwa vizuri zaidi,” alisema Dante.
Mahadhi naye
alisema: “Tulijitahidi kwa kweli kupambana kwa uwezo wetu wote lakini tulikosa
kidogo umakini katika kipindi cha kwanza cha mchezo ambacho ndiyo tulifungwa
mabao yote matatu.”
Post a Comment