TATIZO halipo kwenye ngoma ya
Kidogo ya Diamond Platnumz aliyowashirikisha P Square kutoka Nigeria, lakini ishu
hapa ni video ya wimbo huo ambayo ni kali lakini imeshuka vyeo kutokana na ‘copy
& paste’ iliyotumika.
Siyo siri tena kwamba video
hiyo iliyotoka wiki iliyopita ni kwamba imekuwa na mfanano mwingi wa mavazi na
maudhui kutoka kwenye video tatu tofauti za wasanii wakubwa wa Marekani.
Kilichotokea ni kuwa Diamond
amerudia kitu alichowahi kukifanya katika video ya Make Me Sing aliyoimba na
AKA ambayo kwa kiwango cha juu alikopi video ya Got Money ya Lil Wayne. Kupitia
gazeti hili niliandika juu ya mfanano huo, Februari 19, 2016.
Nikianza na kipande cha mwishoni
mwa video yake ya Kidogo, Diamond anaonekana akiwa na Simba pembeni ya kiti
chake, kipande kama hicho kinapatikana kwenye moja ya kava za ‘series’ ya Empire
inayomuonyesha Terrence Howard akiwa na Simba pembeni kwa mapozi na mavazi
yaleyale.
Utetezi wa Diamond unaweza
kuwa alichotaka ni kuonyesha yeye ni Simba kama anavyojiita lakini uhalisia ni
kuwa alikopi na angeweza kubuni staili yake ambayo ingeweza kuleta mfanano wa
jina la mnyama huyo.
Katika shairi la kwanza
analoanza kuimba Paul Okoye, anaonekana katika meza ya chakula akiwa na mavazi,
meza na viti vyeupe, ‘scene’ ambayo inafanana kila kitu na ile iliyopo katika video
ya For The Road ya Tyga iliyowekwa mtandaoni Mei 24, 2013. Mfanano huo upo hadi
katika ‘frame’ tupu zilizopo kwenye ukuta ndani ya video zote hizo.
Kuna sehemu Tyga anaonekana
akiwa na mbwa mwitu mweupe kwenye makochi meupe, kama kawa Diamond naye anapita
mulemule, tofauti ni kuwa mhusika mmoja ni Mtanzania mwingine ni Mmarekani.
Kuna kipande Peter Okoye anaimba
akiwa juu ya spika, mtazamo wa hapo unaendana kila kitu na video ya That’s Me
Right There ya Jasmine V aliyomshirikisha Kendrick Lamar iliyotoka Agosti 22,
2014.
Kama hiyo haitoshi, wadada
wanaocheza (cheerleaders) kwenye Kidogo wamevaa nguo zinazofanana na wale wa
kwenye Shake It Off ya Taylor Swift iliyotoka Agosti 18, 2014 kuanzia dizaini
mpaka rangi za kijani na bluu za nguo hizo!
Diamond ni msanii anayevuka
kutoka Afrika kuelekea Ulaya na Marekani, sasa kama anawaiga waziwazi kiasi
hicho atakuwa na nguvu gani ya kuwaletea changamoto mpya kwenye ushindani wa
kimataifa na hao anaowaiga kwa kila kitu!
Kufika levo za Tuzo za BET lazima
wahusika watakuwa wanafuatilia kazi za Diamond, inapotokea wanaona vitu kama
hivyo vinaweza kuchangia kumshusha kisanii.
Huu ndiyo mwanzo wa kuonekana
‘hana kitu’ na hata zile za awali alibahatisha au nazo ni za kukopi kazi ambazo
hazijajulikana bado.
Kingine, uongozi wa Baba
Tiffah unaweza kuwanyooshea kidole watengenezaji wa video hiyo, Godfather
Productions kuwa wao ndiyo ‘master mind’ wa kila kitu katika hilo lakini je, ni
wangapi wenye uelewa huo?
Nafikiri kuishiwa au kupoteza
uwezo wa kufikiri ndiyo suala sahihi zaidi hapa, maana ilianza kwenye Make Me
Sing na sasa tunayaona haya. Inajulikana kuwa hata msanii anaruhusiwa kupeleka mwongozo
(script) wa anachokihitaji, sasa nani amefanya nini kati yao (Godfather na
Diamond)?
Diamond eeeh! Kwa hapa
ilipofika inatosha, ikiwezekana badili upepo au ongeza washauri na wajuzi wa
mambo katika masuala ya video watakaoweza kung’amua mambo kabla ya mzigo kwenda
hewani.
Tusidanganyane eti video ya
Kidogo ikifika Amerika itaonekana mpya na kali wakati umeiba mawazo yao na
kuyafanya katika kiwango kilekile au chini ya hapo, ukiiba au ukikopi unatakiwa
ufanye kitu bora na uboreshe zaidi ya kule ulikochukua.
Post a Comment