MSHAMBULIAJI wa Medeama FC, Bernard Danso aliyefunga bao la
kuchomoa la timu hiyo walipoumana na Yanga, ametamba kuwa ameshawasoma mabeki
wa timu hiyo na lazima ataifunga tena Yanga katika mechi ya marudiano huko kwao
Ghana.
Katika mchezo huo wa Kombe la Shirikisho Afrika uliopigwa
Jumamosi iliyopita Uwanja wa Taifa, Yanga ndiyo ilikuwa ya kwanza kupata bao
kupitia kwa Donald Ngoma dakika ya pili lakini halikudumu baada ya Danso
kuchomoa bao hilo dakika ya 19 na kusababisha sare ya bao 1-1 yaliyoiacha mkiani
Yanga katika Kundi A.
“Yanga ni timu nzuri lakini niliwasoma mabeki wao kwa dakika
tano za mwanzo nikiwa uwanjani na kujua nifanye nini, tangu nakuja Tanzania
nilipanga kuwa lazima nifunge na kweli imekuwa hivyo. Najua mechi ya nyumbani
Ghana watanizuia sana lakini lazima nitawafunga tena.
“Lengo letu ni ushindi tu katika mechi zilizosalia na unaona
Yanga ndiyo mechi inayofuata kwa hiyo ni lazima tuhakikishe ushindi kwenye
mechi za mapema ingawa najua wataleta ushindani lakini sidhani kama wataweza
kutuzuia,” alisema Danso aliyefunga mabao nane mpaka sasa kwenye Ligi Kuu ya
Ghana.
Yanga iliyopo mkiani mwa Kundi A ikiwa na pointi moja baada
ya mechi tatu inatarajia kurudiana na Medeama Jumanne inayokuja. Katika Kundi
hilo, TP Mazembe ya DR Congo ndiyo kinara ikiwa na pointi saba, MO Bejaia
(Algeria) ina tano kisha Medeama yenye mbili.
Post a Comment