NAHODHA wa zamani wa timu ya Taifa, Taifa Stars, Juma
Kaseja, ameteuliwa na Shirikisho la Soka nchini (TFF) kuwa kocha msaidizi, pamoja na majukumu mengine ya
ukocha wa makipa katika timu ya taifa ya
vijana wenye umri wa miaka 17, Serengeti Boys.
Kaseja amepewa
nafasi hiyo ya ukocha wa muda baada ya kocha msaidizi wa awali, Sebastian Mkoma
na wa makipa, Muharami Mohamed, kuanza mafunzo
ya ukocha ngazi za juu ikiwemo leseni A.
Akizungumza na
waandishi wa habari msemaji wa Shirikisho hilo, Alfred Lucas, alisema: “Kaseja
amepewa nafasi hiyo kutokana na makocha hao wote wawili wa awali kuanza mafunzo
ya ukocha ya ngazi ya juu leseni A.”
Akizungumzia
uwezo wa Kaseja ambaye atakuwa msaidizi wa Kocha Mkuu, Bakari Shime, Ofisa
Habari huyo alisema: “Kaseja ana uzoefu mkubwa wa soka pia amesomea masuala ya ukocha (intermediate),
hivyo kazi aliyopewa ataimudu vizuri.”
Kikosi hicho
cha Serengeti Boys kimesafiri alfajiri ya jana kikiwa na jumla ya wachezaji 19,
viongozi na benchi la ufundi sita kwenda kuweka kambi ya siku kumi nchini
Madagascar ikiwa ni maandalizi ya mchezo
wa mtoano dhidi ya Afrika Kusini utakaopigwa Agosti 5, mwaka huu nchini Afrika
Kusini, kutafuta tiketi ya kucheza fainali za vijana 2017.
Post a Comment