WAKATI akiendelea kukinoa kikosi
chake kipya cha Simba, Kocha wa timu hiyo Mcameroon, Joseph Omog ameomba
kucheza michezo mitatu ya kirafiki ya kimataifa sawa na dakika 270 kwa ajili ya
kukipima kikosi hicho.
Timu hiyo, hivi sasa ipo Mkoani
Morogoro kwa ajili ya kambi ya pamoja kujiandaa na msimu mpya wa Ligi Kuu Bara
chini ya Mcameroon huyo na Mganda, Jackson Mayanja.
Wakati akiendelea kukinoa kikosi
chake, kocha huyo anaendelea na mchujo wa wachezaji wa kimataifa wanaokwenda
mkoani humo kwa ajili ya majaribio.
Katibu Mkuu wa timu hiyo, Patrick
Kahemele alisema yapo baadhi ya mapendekezo waliyoyapokea kutoka kwa kocha
ikiwemo hilo la kucheza mechi tatu za kirafiki kabla ya kuanza kwa ligi kuu.
Kahemele alisema, kikubwa kocha
anataka kuona sehemu zenye upungufu atakazoziimarisha kabla ya kuanza kwa ligi
kuu na lengo ni kuwa na kikosi imara kitakacholeta ushindani ndani ya uwanja.
"Wakati kocha akiendelea na
program ya fiziki huko Morogoro, tayari tumepokea baadhi ya mapendekezo muhimu ikiwemo
la kuomba kucheza mechi tatu za kirafiki za kimataifa baada ya kumaliza program
hiyo ya fiziki.
"Bado hatujajua tutacheza na
timu gani, hivi sasa tupo kwenye mazungumzo na baadhi ya timu ambazo
tusingependa kuzitaja hadi pale zitakapothibisha kucheza.
"Na hiyo imetokana na nchi hizi
za Afrika kutofautiana vipindi vya maandalizi ya ligi kuu, zipo nyingine ligi
zao zimemalizika na nyingine ambazo zipo kwenye usajili, hivyo hali hiyo
inatupa ugumu kama uongozi, lakini kila kitu tutakiweka wazi hivi karibuni,"alisema
Kahemele.
Post a Comment