SIMBA tayari imekamilika
katika mazoezi ya kujiandaa na msimu ujao wa Ligi Kuu Bara baada ya beki wa
kati wa timu hiyo, Emmanuel Semwanza kurejea kikosini katika kambi ya timu hiyo
huko mkoani Morogoro.
Semwanza aliyesajiliwa hivi
karibuni akitokea Mwadui FC ya Shinyanga, alikuwa mchezaji pekee wa timu hiyo
ambaye hajajiunga na timu hiyo kutokana na kufiwa na mama yake mzazi na hivyo
kupata udhuru wa kuhudhuria mazishi mkoani Mbeya.
Meneja wa timu hiyo, Abbas Ally,
amesema kuwa Semwanza amejiunga na kikosi hicho rasmi juzi baada ya kuwa nje ya
kikosi kwa takriban siku tano, hivyo sasa kikosi hicho kipo kamili katika
maandalizi yao chini ya kocha Mcameroon, Joseph Omog.
“Kambi inaendelea vizuri,
hakuna tatizo lolote zaidi amerejea Semwanza ambaye yeye alikuwa nje ya kikosi
kutokana na msiba, hivyo sasa kikosi kimekamilika katika kuendelea na programu
za mwalimu za kujiandaa na msimu mpya wa ligi,” alisema Abbas.
Mpaka mwisho wa wiki hii
Simba itakuwa imetimiza wiki nne katika kambi hiyo ikiendelea kujifua na
kuwajaribu wachezaji wa kigeni waliopo kikosini humo na kama wakifuzu waingie
kandarasi za kuitumikia timu hiyo msimu ujao, lengo likiwa ni kurekebisha
makosa ya kutoshiriki michuano ya kimataifa kwa misimu minne mfululizo.
Post a Comment