KOCHA Mkuu wa Yanga, Hans van Der Pluijm, ameshusha
presha ya mechi dhidi ya Medeama ya Ghana mara baada ya kuhakikishiwa kuwa
mshambuliaji wake Mrundi, Amissi Tambwe amepona na ni ruksa kumtumia kwenye
mchezo huo.
Yanga iliyoweka kambi yake Bahari Beach Hotel, Dar,
inatarajiwa kuvaana na Medeama, kesho Jumamosi kwenye Uwanja wa Taifa jijini
Dar es Salaam katika mchezo wa Kombe la Shirikisho Afrika.
Akizungumza na Championi Ijumaa, Pluijm alisema
mshambuliaji huyo ana umuhimu mkubwa wa kucheza katika mechi hiyo kutokana na
mfumo anaotarajiwa kuutumia ndani.
Amesema hofu ya kumkosa Tambwe imeisha baada ya mchezaji
huyo kuanza mazoezi mepesi ya binafsi juzi asubuhi kwenye Uwanja wa Boko Beach
Veteran, Dar.
Aliongeza kuwa anaheshimu uwezo wa wachezaji wake wote,
lakini anamhitaji Tambwe kuwepo kwenye kikosi hicho kutokana na kuzoeana na
Ngoma wakiwa uwanjani.
“Daktari wa timu amenihakikishia kuwa ataweza kucheza
mechi hiyo ya Medeama kutokana na maendeleo ya kiafya kuwa vizuri.
“Ninaamini uwepo wake kwenye timu utachangia ushindi wa
mchezo kutokana na umuhimu wake kwenye timu,” alisema Pluijm.
Upande wa Tambwe alipoulizwa juu ya afya yake na mchezo
huo wa kesho, alisema: “Nashukuru ninaendelea vizuri, hatma yangu ya kucheza namuachia
kocha, lakini mimi nimepona na ningetaka kucheza katika mechi hiyo ambayo
lazima tuwafunge kwa staili yoyote ili kuhakikisha tunatimiza ahadi yetu ya
kufika nusu fainali ya michuano hiyo.”
Post a Comment