YANGA na Medeama ya Ghana ni kesho Jumamosi lakini Kocha
wa Yanga, Hans van Der Pluijm amewaambia wachezaji wake kuwa anataka kuona muda
wote wanacheza kwenye eneo la wapinzani wao hao wakiwashambulia.
Timu hizo zinakutaka katika mchezo wa hatua ya makundi ya
Kombe la Shirikisho Afrika kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam ambapo
ushindi pekee ndiyo utakaoamsha matumaini ya kusonga mbele.
Pluijm ameyasema hayo alipokuwa katika mazoezi ya timu
yake juzi, ambapo alionekana kuwa bize akitoa mbinu za jinsi ya kushambulia.
Katika mazoezi hayo yaliyofanyika kwenye Uwanja wa Boko
Veterani, Dar, Pluijm alikuwa akitaka wachezaji wanapokuwa kwenye nusu yao waguse
mpira mara moja na kutoa pasi, lakini wanapovuka mstari wa kati wanatakiwa kuwa
huru kuuchezea mpira watakavyo huku wakitengeneza nafasi za kufunga.
Zoezi hilo lililodumu kwa takribani dakika 20, lilienda
vizuri hali iliyomfurahisha Pluijm ambapo baadaye alisema kuwa lazima wafanye
hivyo kutokana na kwamba staili hiyo inamlazimu mpinzani wako kukaa zaidi katika
eneo lake na kukupa nafasi ya kumshambulia.
“Unapotaka kumshinda mpinzani wako ni lazima umlazimishe
abaki kwenye eneo lake ndiyo maana nataka kwenye mechi tucheze zaidi kwenye
eneo la wapinzani kuliko kwetu.
“Sitaki kuona tunacheza sana kwetu na badala yake muda
wote tuwe kwa wapinzani.
“Lakini pia nataka tufanye kama ilivyokuwa kwenye ligi,
muda mwingine tulikuwa tunaanza kufungwa lakini tunajipanga na kurudisha na
hatimaye kuibuka na ushindi, sasa hali hiyo nataka pia tufanye kwenye michuano
hii ya kimataifa,” alisema Pluijm.
Wakati
huohuo, mshambuliaji wa Yanga, Mzimbabwe, Donald Ngoma amedai kuwa hataki kuona
wala kusikia suala la kufungwa katika mchezo huo.
“Hatujafunga
na hatuna pointi yoyote jambo ambalo siyo zuri kwetu, nafikiri tukifanya vizuri
katika mechi hiyo itatufanya tufufue matumaini. Tutapambana kwa muda wote,”
alisema Ngoma.
Post a Comment