Dar es Salaam,Tanzania.
TIMU ya Simba imepoteza matumaini ya kuinasa saini ya
mshambuliaji wa kimataifa wa Burundi, Laudit Mavugo baada ya jina la mchezaji
huyo kuwemo kwenye orodha ya kikosi cha timu yake ya Vital’O kitakachoshiriki
Ligi Kuu ya nchi hiyo msimu ujao.
Uongozi wa Simba ukiongozwa na Mwenyekiti wa Kamati ya
Usajili Zacharia Hanspoppe, uliahidi kumleta Msimbazi mshambuliaji huyo mwenye
kulijua vizuri lango la timu pinzani, baada ya kushindwa kufanya hivyo msimu
uliopita.
Kwa mujibu wa vyombo vya habari kutoka Burundi, jina la
Mavugo ni miongoni mwa majina 29 ya wachezaji waliosajiliwa na Vital’O, kwa
ajili ya kuitumikia timu hiyo na tayari usajili huo umeshawasilishwa kwenye
shirikisho la soka la nchi hiyo, FFB.
Akizungumza jana Hanspoppe alisema walikuwa na mazungumzo na
mchezaji huyo pamoja na klabu yake ya Vital’O na wanashangazwa na taarifa hizo
za jina lake kuwemo kwenye orodha ya wachezaji watakaoitumikia timu hiyo msimu
ujao.
“Inashangaza kusikia
taarifa hizo lakini kama Simba hatutakata tamaa tutaendelea na jitihada zetu za
kumsajili kwa kukutana na viongozi wa timu yake na yeye mwenyewe hadi mwisho
naamini hakuna kinachoshindikana ukizingatia muda wa usajili bado upo,”alisema
Hanspoppe.
Mavugo alikuwa chaguo la kwanza la Simba kwenye usajili wa
msimu huu ingawa baadaye miamba ya Kenya, Gor Mahia waliingilia kati mbio hizo
nao wakiiwania saini ya Mrundi huyo ambaye ana sifa ya kucheka na nyavu.
Post a Comment